Sunday 7 December 2014

BENKI YA NMB, TAWI LA SINGIDA IMESHEREHEKEA SIKU YA KUJUMUIKA NA WAFANYAKAZI WOTE, 'NMB FAMILY DAY', KWA AMANI, NA KUFANA KWA KIWANGO KIKUBWA, HUKU WAFANYAKAZI WAKE WAKILA, KUNYWA NA KUFURAHIA KUPITIA MICHEZO MBALIMBALI

SHEREHE KWA WAFANYAKAZI WA BENKI YA NMB, TAWI LA SINGIDA JINSI ZILIVYOFANA KATIKA VIWANJA VYA HOTELI YA KBH, ILIYOPO ZIWA SINGIDANI.
BENKI ya NMB, Tawi la Singida imefanya sherehe kubwa kwa ajili ya siku ya wafanyakazi wake, ‘NMB Family’, iliyofanyika katika hotel ya KBH mjini Singida na kufana kwa kiwango kikubwa. Licha ya familia hizo kukutana pamoja, pia yalifanyika mashindano mbalimbali, ikiwemo kufukuza kuku (wanaume na wanawake), mpira wa miguu (wanaume) na muziki (dansi) kwa watoto. Hata hivyo watoto wawili wa mtumishi wa benki hiyo, Bw. Joseph, walifanikiwa kushinda baada ya kusakata vyema muziki wa kizazi kipya na kupewa zawadi mbalimbali na meneja wa tawi hilo, Bibi.Christine Mwangomo. MWISHO

BENKI YA NMB, TAWI LA SINGIDA IMEKABIDHI WATEJA WAKE WAWILI ZAWADI YA BAISKELI, BAADA YA KUSHINDA SHINDANO LILILOANZISHWA NA BENKI HIYO KWA AJILI YA WATEJA WANAOWEKA FEDHA KUPITIA AKAUNTI ZAO, KWENYE BENKI HIYO

MENEJA wa benki ya NMB, Tawi la Singida Bibi. Christine Mwangomo (kulia, akimpa mkono wa hongera mmoja wa wateja kati ya wawili, walioshinda shindano na weka ushinde (mwingine aliyeshinda ni mwanamke lakini hayupo kwenye picha), baada ya kuweka fedha kwenye akaunti yake na kujishindia baiskeli mpya. katikati ni meneja msaidizi wa tawi hilo, Bw. Makoyi.

MBUNGE VITI MAALUMU (CCM) MKOA WA SINGIDA, MARTHA MLATA AMEISAIDIA SEKONDARI YA NDUGUTI SH.MILIONI TATU KUONDOA TATIZO LA MAJI SHULENI HAPO

MBUNGE viti maalumu (CCM) Mkoa wa Singida, Martha Mlata ametoa msaada wa shilingi milioni tatu kwa sekondari ya kata ya Nduguti, wilaya ya Mkalama mkoani Singida, kwa ajili kuodoa tatizo la maji linaloikabili shule hiyo kwa muda mrefu sasa. Alilazimika kutoa kiasi hicho, baada ya kusomwa risala kwenye mahafali ya sita ya shule hiyo, kwamba inakabiliwa na changamoto nyingi, mojawapo ikiwa ni tatizo la maji, ambalo husababisha wanafunzi kupoteza muda mwingi kusaka maji, badala ya kushiriki masomo. Hata hivyo Mlata aliitaka halmashauri ya wilaya ya Mkalama kuhakikisha nayo inachangia kiasi cha fedha kitakachopungua, ili kazi ya kuvuta maji kwa kutumia mtandao wa bomba iweze kukamilika haraka, na yeye akabidhiwe mapema januari mwakani wakati shule zitakapofunguliwa. Licha ya kutoa kiasi hicho cha fedha, Mlata alikabidhi pia mipira na jezi za mchezo wa soka, kwa ajili ya wasichana na wavulana wa shule hiyo, msaada uliogharimu zaidi ya Sh.laki mbili na nusu. MWISHO.

SERIKALI YA MKOA WA SINGIDA IMETAKIWA KUMALIZA HARAKA MIGOGORO YA MIPAKA ILI KUWEZESHA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA HAPO DISEMBA 14, 2014, KUFANYIKA KWA AMANI

Na Elisante John, Singida SERIKALI imetakiwa kutatua migogoro ya mipaka, ili kufanikisha zoezi la uchaguzi wa serikali za mitaa, utakaofanyika disemba 14, 2014. Rai hiyo imetolewa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida, kupitia mwenyekiti Mgana Msindai na katibu wake Mary Chatanda, wakati wa kikao cha kamati ya ushauri cha Mkoa. “Mheshimiwa mwenyekiti, iwapo tatizo hili litaondolewa, nina uhakika wananchi wetu watashiriki vyema zoezi la uchaguzi wa serikali ya mitaa, utakaofanyika hivi karibuni,”alisema Chatanda. Msindai alibainisha kuwa, tatizo hilo limekithiri mkoani Singida, kuanzia ngazi ya kitongoji, vijiji, kata, wilaya, pia kati ya mkoa wa Singida na baadhi ya majirani zake, ikiwemo wilaya ya Uyui, mkoani Tabora. Aliiomba serikali kumaliza haraka tatizo hili, ili wananchi waweze kushiriki vyema uchaguzi wa serikali za mitaa, ambao baadhi ya wananchi wapo hatarini kupiga kura, kutokana na kukithiri kwa migogoro hiyo. Aidha mbunge viti maalumu (CCM) Mkoa Singida, Mathar Mlata aliomba fedha za upimaji ardhi zinapopatikana kwa kila halmashauri, zikafanye kazi katika maeneo ya vijiji, badala ya kuanza na makao makuu ya wilaya. Makamu mwenyekiti halmashauri wilaya Singida, Elia Digha aliitaka serikali kutatua mgogoro wa mpaka, kati ya manispaa Singida na wilaya yake, katika eneo la Njiapanda, ambako kuna mnada maarufu, kila siku ya jumamosi. Akijibu hoja hiyo, katibu tawala mkoa Singida, Liana Hassan alisema serikali inatambua tatizo hilo, akawaomba wajumbe kuvumilia wakati huu, ambao jitihada zinafanyika, ili kutatua kero hiyo. “Tatizo hili limekuwa likishughulikiwa kwa muda sasa…nawaomba sana wajumbe muendelee kuwa wavumilivu, baada ya uchaguzi utatuzi wa migogoro hii itakuwa imepatiwa ufumbuzi,”alisema. Akihitimisha, mkkuu wa mkoa wa Singida, Dk. Parseko Kone aliagiza wakuu wa wilaya na sekretarieti ya mkoa kumaliza tatizo hilo haraka, pia mgogoro wa mpaka kati ya wilaya za Manyoni (Singida) na Sikonge (Tabora). MWISHO.