Sunday 7 December 2014

SERIKALI YA MKOA WA SINGIDA IMETAKIWA KUMALIZA HARAKA MIGOGORO YA MIPAKA ILI KUWEZESHA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA HAPO DISEMBA 14, 2014, KUFANYIKA KWA AMANI

Na Elisante John, Singida SERIKALI imetakiwa kutatua migogoro ya mipaka, ili kufanikisha zoezi la uchaguzi wa serikali za mitaa, utakaofanyika disemba 14, 2014. Rai hiyo imetolewa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida, kupitia mwenyekiti Mgana Msindai na katibu wake Mary Chatanda, wakati wa kikao cha kamati ya ushauri cha Mkoa. “Mheshimiwa mwenyekiti, iwapo tatizo hili litaondolewa, nina uhakika wananchi wetu watashiriki vyema zoezi la uchaguzi wa serikali ya mitaa, utakaofanyika hivi karibuni,”alisema Chatanda. Msindai alibainisha kuwa, tatizo hilo limekithiri mkoani Singida, kuanzia ngazi ya kitongoji, vijiji, kata, wilaya, pia kati ya mkoa wa Singida na baadhi ya majirani zake, ikiwemo wilaya ya Uyui, mkoani Tabora. Aliiomba serikali kumaliza haraka tatizo hili, ili wananchi waweze kushiriki vyema uchaguzi wa serikali za mitaa, ambao baadhi ya wananchi wapo hatarini kupiga kura, kutokana na kukithiri kwa migogoro hiyo. Aidha mbunge viti maalumu (CCM) Mkoa Singida, Mathar Mlata aliomba fedha za upimaji ardhi zinapopatikana kwa kila halmashauri, zikafanye kazi katika maeneo ya vijiji, badala ya kuanza na makao makuu ya wilaya. Makamu mwenyekiti halmashauri wilaya Singida, Elia Digha aliitaka serikali kutatua mgogoro wa mpaka, kati ya manispaa Singida na wilaya yake, katika eneo la Njiapanda, ambako kuna mnada maarufu, kila siku ya jumamosi. Akijibu hoja hiyo, katibu tawala mkoa Singida, Liana Hassan alisema serikali inatambua tatizo hilo, akawaomba wajumbe kuvumilia wakati huu, ambao jitihada zinafanyika, ili kutatua kero hiyo. “Tatizo hili limekuwa likishughulikiwa kwa muda sasa…nawaomba sana wajumbe muendelee kuwa wavumilivu, baada ya uchaguzi utatuzi wa migogoro hii itakuwa imepatiwa ufumbuzi,”alisema. Akihitimisha, mkkuu wa mkoa wa Singida, Dk. Parseko Kone aliagiza wakuu wa wilaya na sekretarieti ya mkoa kumaliza tatizo hilo haraka, pia mgogoro wa mpaka kati ya wilaya za Manyoni (Singida) na Sikonge (Tabora). MWISHO.

No comments:

Post a Comment