Sunday 11 May 2014

ELIMU INAWEZA KUMKOMBOA BINADAMU, HASA KAMA ATAZINGATIA IPASAVYO MASOMO YAKE. JULIUS CHARLES NI MWANAFUNZI WA DARASA LA SITA ANAYETUMIA MGUU WAKE WA KULIA KUANDIKA DARASANI KUTOKANA NA ULEMAVU ALIONAO WA MIKONO.

WANAFUNZI wa Shule ya Msingi Ikungi Mchanganyiko, kitengo cha walemavu (wasioona) wakiwa darasani kuendelea na masomo chini ya walimu wao.
MWANAFUNZI Julius Charles mlemavu wa mikono, akiwa darasani huku akiandika kwenye daftari lake kwa kutumia vidole vya mguu wake wa kulia.
Julius akitandika kitanda chake kwa kutumia mguu wake wa kulia.
Akiwa kwenye darasa la kawaida (mbele aliyeweka daftari chini huku akiandika),pamoja na wanafunzi wenzake wasiokuwa na ulemavu.
Julius akitoka darasanibaada ya kumaliza kipindi na wanafunzi wenzake wasiokuwa na ulemavu.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Olvary Kamilly akiwa ofisini kwake, akizungumza na mwandishi wa habari hizi (hayupo pichani), alisema jamii ya walemavu inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo wazazi kuwaficha majumbani, pia kuwahudumia watu wa aina hii ni gharama kubwa na akaiomba jamii kuisaidia shule hiyo kwa hali na mali.
Singida. Mei 12, 2014. KUNA methali isemayo ‘Shida huleta maarifa’ na ‘Kama hujafa hujaumbika.Julius Charles (12) ni mlemavu wa viungo, anayesoma shule ya msingi Ikungi mchanganyiko, iliyopo Wilaya Ikungi, Mkoani Singida. Ni mlemavu wa mikono, lakini kutokana na bidii darasani ameweza kumudu vyema kusoma na kuandika, hali inayomwezesha awazidi hata wenzake wazima anaosoma nao darasa la sita. Alianza elimu ya msingi mwaka 2006 kwa msaada wa mama yake aliyepata taarifa juu ya shule hiyo yenye kuchukua wanafunzi Mchanganyiko (yaani wenye afya njema) na walemavu ambao wanaishi bweni. Julius alizaliwa kijiji cha Mgungari Wilaya Bunda mkoani Mara mwaka 2002, ni mtoto wa kwanza wa bwana na bibi Charle Namwanga, lakini baba yake aliugua ugonjwa wa akili, hivyo kumtegemea zaidi mama yake, serikali na wahisani kupata mahitaji muhimu. Anamudu vyema masomo yake kutokana na ushirikiano wa walimu tangu akiwa darasa la kwanza, na sasa wenzake na walimu humsaidia kwa kukamatisha kalamu kwenye mguu wa kulia, naye huandika vyema hata kuwazidi wengine wenye mikono kamili. Licha ya kufanya vyema darasani na kushika nafasi ya tatu kati ya wanafunzi 62, Julius pia humudu kuoga na kufanya kazi nyinginezo ndogondogo, ikiwemo kutandika kitanda, lakini anatoa somo kwa walemavu kujiendeleza kimasomo ili baadaye wajikomboe kiuchumi. Kama walivyo watu wengine wenye malengo ya baadaye, ndoto ya Julius ni kuwa mwanasiasa aliyebobea, ili aweze kuwasemea walemavu wenzake akiwa bungeni. Olivary Kamilly ni mwalimu mkuu wa shule hiyo, anasema Julius ni mwanafunzi anayezingatia masomo na hushiriki madarasa yote mawili, akianza na la kawaida, kisha baadaye darasa la walemavu, ingawa pia changamoto zipo nyingi zinazoikabili shule hiyo. Mwalimu Kamilly anaiomba jamii kuacha kuwatenga watoto wenye ulemavu, badala yake wawathamini na wajitahidi kuwasomesha katika shule maalumu, ili baadaye waweze kukidhi matarajio yao. Pia ameiomba jamii kuisaidia shule hiyo ili iweze kumudu vyema kuwahudumia wanafunzi wenye matatizo ya ulemavu. Adamu Bilali ni mwalimu mlemavu wa macho na Anna Mjema ni mwalimu wa wanafunzi wenye ulemavu katika shule hiyo, wanasema kuwa jamii hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo ugumu wa kufundisha mlemavu kama huyu. MWISHO.

No comments:

Post a Comment