Wednesday 7 May 2014

HALMASHAURI YA WILAYA MKALAMA YAPITISHA TASIMU YA SHERIA NDOGO KWA AJILI YA ADA NA USHURU KUONGEZA UFANISI WA UTEKELEZAJI WA KAZI ZAKE.

MWENYEKITI wa halmashauri Wilaya Mkalama Mkoani Singida James Mkwega akisisitiza jambo wakati wa maamuzi juu ya kupitisha rasimu ya sheria ndogo mbalimbali,ikiwemo ushuru wa kuku, samaki na mazao, wakati wa baraza la madiwani lililokutana makao makuu ya Wilaya hiyo, Nduguti.
Mwanasheria wa halmashauri ya Wilaya Mkalama Neto Mwambalasu akiwasilisha rasimu ya sheria ndogo ya ada na ushuru mbalimbali mbele ya baraza la madiwani kwenye kikao cha baraza hilo lililokutana makao makuu ya wilaya hiyo, Nduguti.
Baadhi ya madiwani wa halmashauri ya Wilaya Mkalama wakipitia makablasha yenye taarifa mbalimbali ikiwemo rasimu ya sheria ndogo kwa ajili ya ada na ushuru wa kuku, mazao na samaki ili kuiongezea halmashauri hiyo uwezo wa kutekeleza majukumu yake.
Singida Mei 07, 2014. ILI kuiongezea uwezo halmashauri ya wilaya Mkalama Mkoani Singida itaanza kutoza ushuru wa kuku,samaki na mazao mbalimbali. Mwanasheria wa halmashauri hiyo Neto Mwambalasu aliwaeleza wajumbe wa mkutano wa baraza la madiwani lililokutana Nduguti kuwa, utekelezaji wa ushuru huo utaanza kutozwa baada ya kusainiwa na waziri mwenye dhamana, waziri mkuu Mizengo Pinda. Hata hivyo baadhi ya madiwani walionyesha wasiwasi kuhusiana na ushuru wa kuku, lakini mwansheria huyo aliwatoa mashaka kwa maelezo kuwa, sana sheria hiyo itawahusu wafanyabiashara wanaonunua na kusafirisha au kuvusha nje ya Wilaya hiyo. “Nawaomba sana waheshimiwa msipate wasiwasi kuhusiana na rasimu hii…mfano!, ushuru wa kuku wa Sh.500 kwa kuku, hautamhusu moja kwa moja mwananchi wa kawaida, badala yake utahusisha zaidi wafanyabishara wanaonunua na kusafirisha kuku wengi, kwa ajili ya biashara,”alifafanua. Mazao mengine yanayoingia kwenye rasimu na kiwango kikiwa katika mabano ni, samaki aina ya perege (Sh. 300), kambale (Sh. 50), kamongo (Sh.50), ng’ombe, nguruwe na punda (Sh. 2,000), wakati mbuzi na kondooo watalazimika kulipiwa ushuru wa Sh.1,000, kwa mmoja. Kwa mujibu wa Mwansheria huyo, baadhi ya ada na ushuru huo mwingine utakaohusisha maeneo 18, ni mazao ya chakula na biashara, vizimba sokoni, machinjio, ushuru wa madini, ada ya idhini ya ujenzi, mazao ya nyuki na ushuru wa kupaki/kuegesha magari. Katika hatua nyingine, baraza hilo lilipitisha mapendekezo ya kuyagawanya baadhi ya maeneo kwa kuyapandisha hadhi, ikiwemo vitongoji, vijiji, kata na tarafa, ili kutoa fursa kwa wananchi kunufaika na huduma bora baada ya kusogezwa karibu zaidi. Baadhi ya maeneo yaliyopendekezwa kuwa kata ni Mkalama, Nkalakala, Kidarafa, Tatazi, Lukomo, Tumuli, Lyelembo, Ikungu, Kinampundu, Nkungi, Dominiki na Endasiku, wakati tarafa zitakazoongezeka ni Mwanga, Gumanga na Mkalama (iliyobadilishwa kutoka Ibaga kuwa Mkalama). MWISHO.

No comments:

Post a Comment