Monday 5 May 2014

KLABU YA WAANDISHI WA HABARI MKOA WA SINGIDA-SINGPRESS IMEKABIDHI MSAADA WA KIBINADAMU KWA SHULE MAALUMU YA IKUNGI MCHANGANYIKO YENYE WALEMAVU WA AINA MBALIMBALI WAPATAO 104

MWALIMU mkuu wa shule ya msingi Ikungi Mchanganyiko iliyopo wilaya Ikungi Mkoani Singida, Bw. Olvary Kamilly (kulia) akipokea sehemu ya msaada kutoka kwa mwenyekiti wa klabu ya waandishi wa habari mkoa Singida ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya uhuru wa vyombo vya habari duniani, wakati klabu hiyo ilipoamua kuadhimisha kwa kusaidia shule hiyo yenye wanafunzi 1,200, kati yao 104 wenye ulemavu aina mbalimbali. Msaada huo umejumuisha vitu mbalimbali ikiwemo sukari, unga wa sembe, ngano, kalamu, madaftari, ndoo za maji, mafuta ya kula, biskuti, pipi, sabuni za kufulia, sahani, vikombe nk, katika makabidhiano yaliyofanyika shuleni hapo.
Elisante John, Singida Mei, 2014. WALEMAVU wamekuwa wakinyanyaswa, kubaguliwa hata kutengwa kutokana na mwonekano wao tu tangu kuzaliwa, lakini katika kukabiliana na tatizo hili serikali imekuwa ikiwapatia elimu kuanzia shule ya awali hadi elimu ya juu, lengo ni kuiwezesha jamii hiyo kupata fursa zaidi ya ajira ndani na nje ya nchi. Shule ya msingi Ikungi mchangayiko iliyopo Wilaya Ikungi Mkoani Singida ni kati ya shule hizo chache za bweni nchini inayotoa taaluma kwa walemavu mbalimbali, wakiwemo wasioona, albino na viungo. Mwalimu mkuu wa shule hiyo Olvary Kamilly anawaeleza wanahabari wa Mkoa Singida waliofika shuleni hapo kukabidhi msaada wa kibinadamu uliogharimu zaidi ya Sh.laki nane, kama sehemu ya maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani kuwa kitengo hicho kilianzishwa mwaka 1980. Kamilly anasema kuwa shule hiyo pia inajumuisha wanafunzi wasiyo walemavu, ambao jumla yao kwa pamoja wanafikia wanafunzi 1,200, wakiwemo wavulana 458 na wasichana 646, huku walemavu pekee idadi yao ni 104. Alisema kati ya wanafunzi hao, Jumanne Ramadhani ni mlemavu wa macho na Julius Charles mlemavu wa mikono (hana kabisa mikononi), lakini ameonyesha uhodari mkubwa wa kuandika kwa kutumia miguu yake, huku Jumanne akisoma kwa ufasaha kwa kupapasa maandishi. Kwa upande wake Mwenyekiti wa klabu ya waandishi wa habari mkoani Singida Seif Takaza alipongeza jitihada zinazofanywa na walimu na wanafunzi wa shule hiyo katika kuhakikisha jamii ya walemavu inaandaliwa kwa ajili ya kukabili maisha ya kujitegemea siku za usoni. Takaza alisema kuwa msaada huo kutoka kwa wanahabari wa mkoa wa Singida ni mwendelezo wa klabu hiyo kusaidia watu wa makundi mbalimbali maalumu yanayoodhani kuwa yametengwa na jamii. Naye Juma Issah ambaye ni mwanafunzi mlemavu wa ngozi, kwa niaba ya wenzake wote aliwashukuru wanahabari wa mkoa wa Singida kutokana na ukarimu waliouonyesha mpaka wakachukua uamuzi wa kushirikiana nao katika maadhimisho hayo. Msaada huo, unga wa sembe, ngano, sabuni, mchele, madaftari, kalamu, mafuta ya kula, pipi, biskuti, sahani, vikombe,ndoo nk, ikiwa ni mwendelezo wa wanahabari hao kusaidia makundi maalumu, kama walivyofanya hivyo mwaka juzi kwa kusaidia jamii ya Wahdzabe, inayoishi wilaya ya Mkalama. MWISHO.

No comments:

Post a Comment