Thursday 1 May 2014

RAIS MSTAAFU AWAMU YA TATU BENJAMEN MKAPA, KUPITIA MFUKO WAKE WA TAASISI YA BENJAMIN MKAPA HIV.AIDS AMEKABIDHI NYUMBA 30 ZA WATAALAMU WA AFYA VIJIJINI MKOANI SINGIDA ZILIZOGHARIMU SH. 1,945,187,143

RAIS wa awamu ya tatu Benjamen Mkapa (katikati) mkuu mkoa Singida Dk. Parseko Kone (kushoto) na mwakilishi wizara ya afya na ustawi wa jamii Dk. Catherine Joachim, akizindua nyumba ya watumishi wa afya vijijini, kati ya 30 zilizogharimu zaidi ya Sh. Bilioni 1.9 kupitia mfuko wa ‘Mkapa Foundation’ kwa wilaya za Mkalama, Iramba, Singida, Ikungi na Manyoni Mkoani Singida.
Mkuu Mkoa Singida Dk. Parseko Kone akikabidhi hati ya nyumba kwa mganga mkuu Wilaya Iramba Dk.Japhet Simeo, baada ya rais mstaafu Benjamen Mkapa kukabidhi nyumba 30 za kisasa kwa ajili ya watumishi wa afya vijijini, zilizojengwa na taasisi ya Mkapa foundation, kwa wilaya za Mkalama, Iramba, Manyoni, Ikungi na Singida, kwenye makabidhiano yaliyofanyika kijiji cha Senenemfuru katika halmashauri ya wilaya Singida.
Rais awamu ya tatu, Benjamen Mkapa akikabidhiwa kibuyu na akina mama wa kijiji cha Senenemfuru Singida vijijini, kikiwa na maana ya upendo, kwenye hafla ya kukabidhi nyumba, kati ya 30 zilizojengwa na Mkapa foundation kwa halmashauri tano za mkoa wa Singida.
Mwonekano wa nyumba iliyojengwa na taasisi ya Benjamen Mkapa katika kijiji cha Senenemfuru halmashauri ya wilaya Singida, kati ya 30 zilizojengwa katika wilaya tano mkoani Singida kwa ajili ya watumishi wa afya vijijini kwa gharama ya Sh.1,945,187,143.
Na Elisante John, Singida April 01, 2014. RAIS mstaafu awamu ya tatu Benjamen W. Mkapa kupitia taasisi yake ‘Benjamen William Mkapa HIV/AIDS’ (BMAF), amekabidhi nyumba 30 zilizojengwa kwenye zahanati 13 na vituo vya afya viwili kwa gharama ya zaidi ya Sh. Bilioni 1. 9, katika halmashauri tano za Wilaya Mkoani Singida. Akikabidhi sehemu ya nyumba hizo kwenye hafla iliyofanyika kijiji cha Senenemfuru Singida vijijini, mzee Mkapa alishukuru wafadhili waliowezesha kazi hiyo, ukiwemo mfuko wa dunia wa kupambana na Ukimwi, kifua kikuu na malaria (Global fund), kwa kuonyesha imani na serikali ya Tanzania. “Binafsi ninafarijika kufahamu kwamba wananchi wanaohudumiwa na zahanati 15 ambazo nyumba hizi zimejengwa, wataendelea kufaidika na huduma bora za afya kutoka vituo hivyo kwa sababu watoa huduma wameboreshewa mazingira ya kazi zao,”alisema rais mstaafu. Nyumba hizo zimejengwa katika zahanati ya Misughaa na Mangonyi (Ikungi), Mkenge, Mpambaa na Senenemfuru (Singida), Ulemo Uwanza na kituo cha afya Ndago (Iramba), Kinyambuli na Dominiki (Mkalama), pia kituo cha afya Itigi, Idodyandole, Heka, Mpola na Chibumagwa (Manyoni). Baada ya kukabidhi, mzee Mkapa alitumia fursa hiyo kuhimiza halmashauri za wilaya husika kutunza vyema nyumba hizo na kutumika kwa matumizi yaliyokusudiwa na alizitaka kutenga bajeti ya kutosha kwa ajili ya matengenezo ya mara kwa mara ili zidumu, kuendelea kuwa madhubuti na kuvutia zaidi. “Hata hivyo, ili kuweza kuwa na huduma ya afya bora zaidi na kamilifu ni lazima kuwepo na zahanati yenye dawa, vifaa vya kutolea huduma na vipimo na uwepo wa wataalamu wa kutosha kulingana na ikama…wekeni mkakati kuhakikisha hayo yote yanazingatiwa na kutekelezwa,”alisisitza Mkapa. Kwa upande wake mwakilishi wizara ya afya na ustawi wa jamii Dk. Catherine Joachim aliishukuru taasisi hiyo na akasema kupitia mradi huo kwa mwaka wa pili sasa utahusisha ujenzi wa nyumba 220 za watumishi wa afya kwa mikoa ya Arusha, Ruvuma, Manyara, Pwani na Singida. Aliishukuru taasisi ya Mkapa kutekeleza kazi zake kwa ushirikiano mkubwa na serikali, mashirika binafsi, wadu wa maendeleo na jamii kwa ujumla, ikiwa na lengo la kuimarisha huduma za Ukimwi, afya ya mama na mtoto na masuala mengine ya afya kwa wataalamu waliopo maeneo ya vijijini. Aidha, afisa mtendaji mkuu wa taasisi Benjamen Mkapa Dk. Ellen Mkondya-Senkoro alisema kuwa BMAF mkoani Singida imekuwa ikichangia shughuli mbalimbali ikiwemo kuimarisha huduma za Ukimwi, afya ya uzazi na masuala ya watumishi wa afya tangu mwaka 2006. Aliyataja mafanikio mengine mkoani hapa kuwa ni pamoja na kuajiri watumishi wa afya 28, kufadhili wanafunzi tisa wanaosoma vyuo mbalimbali vya afya, kujenga wodi ya wazazi katika vituo vya afya, kusaidia magari matatu ya kubebea wagonjwa na kutoa mafunzo juu ya usimamizi wa raslmali watu. MWISHO.

No comments:

Post a Comment