Tuesday 29 April 2014

BASI LA KAMPUNI YA SUMRY LAPARAMIA NA KUUA WATU 19 WAKIWEMO ASKARI POLISI WANNE WALIKOKUWA KAZINI.

PICHA ZA Miili ya askari polisi wanne wa mkoa wa Singida, Boniface Magubika, Novatus Tarimo, Michael Mwakihaba na Jumanne Mwakihaba, ikiwa kwenye masanduku kwa ajili ya ibada ya kuagwa na mamia ya wakazi wa mji wa Singida kwenye viwanja vya line Polisi, tayari kwa kusafirishwa jana jioni kwenda kuzikwa katika mikoa yao walikozaliwa ikiwemo Kilimanjaro, Pwani, Iringa na Mbeya.
Na Elisante John, Singida Aprili 29, 2014. WATU 19 wamekufa, wakiwemo askari polisi wanne na wengine nane wamejeruhiwa vibaya baada ya kugongwa na basi la lililokuwa linatokea Mkoani Kigoma, kwenye eneo la kijiji cha Utaho Kata ya Puma Wilayani Ikungi, barabara kuu ya Sindida- Dodoma kilomita 15 kutoka Singida Mjini. Ajali hiyo ilitokea juzi usiku saa 2.45 na kulihusisha basi namba T 799 BET Nissan mali ya Kampuni ya Sumry, likitokea Kigoma kwenda jijini Dar es Salaam, likiendeshwa na Paulo Njilo mkazi wa jijini Dar es Salaam. Kamanda wa polisi Mkoa Singida Geofrey Kamwela alisema siku ya tukio hilo wananchi wakiwa na askari polisi wa doria walikuwa wamekusanyika pembezoni mwa barabara kuupakia mwili ya mtu mmoja mwendesha baiskeli aliyegongwa na lori na kufariki dunia. Alisema kuwa wakiwa katika harakati za kuupakia mwili huo kwenye gari la polisi namba PT 1424 huku likiwa limeegeshwa pembeni mwa barabara, gafla basi hilo lilikuja kwa kasi na kuwagonga wananchi hao na 15 dunia papo hapo, huku wengine watatu wakifariki dunia wakati wakipelekwa hospitalini. Akielezea tukio hilo, Kamwela alisema dereva wa basi baada ya kukaribia eneo hilo aliliona gari la polisi likiwa limepaki pembeni kushoto mwa barabara, lakini katika kulikwepa ndipo alipoparamia kundi la watu waliokuwa pamoja na askari na kuwagonga huku wengine wakipotez amaisha. Aidha alisema dereva wa basi hilo baada ya ajali hiyo aliendelea na mwendo hadi aliposimama kilomita 25 katika makao makuu ya wilaya Ikungi na kutokomea kusikojulikana, lakini juhudi za kumtafuta zinaendelea. Aliwataja askari waliokufa kuwa ni F.849 D/CPL Boniface Magubika wa CID Wilaya ya Singida, F.6837 Pc Jumanne Mwakihaba wa FFU Singida, G.7993 Pc, Novatus Tarimo wa ofisi ya RCO na G.8948 Pc, Michael Mwakihaba wa FFU Singida. Wengine waliokufa aliwataja kuwa ni afisa mtendaji kijiji cha Utaho Ramadhan Mjengi, Mwenyekiti wa kijiji Utaho Paul Hamis, Mwenyekiti wa kitongoji cha Utaho Ernet Salanga, Said Rajab, Usirika Itambu, Chima Mughenyi, Salim Juma, Abeid Ramadhan, Mwinyi Hamis, na Issa Hussein wote wakazi wa kijiji cha Utaho. Kamanda Kamwela alisema miili ya marehemu wengine wanne bado haijatambuliwa na ndugu zao na imehifadhiwa kwenye chumba cha maiti hospitali ya mkoa wa singida. Alisema majeruhi wawili wamelazwa katika hospitali ya Mkoa Singida na wengine sita wapo hospitali ya misheni Malikia wa Ulimwengu iliyopo Puma. Aidha miili ya askari polisi wote inatarajiwa kusafirishwa kwenda katika mikoa wanakotoka wakati wowote mara taratibu za kipolisi zitakapokamilika, ikiwa ni baada ya kuwasiliana na ndugu zao wa Rombo-Kilimanjaro, Pwani, Mbalizi Mbeya na Iringa. Akielezea ajali hiyo Kamanda Kamwela alisema awali majira ya sa 1:30 usiku ilitokea ajali ya mtembea kwa miguu Gerad Zefania aliyegongwa na lori na kufa papo hapo. Mmoja wa majeruhi aliyelazwa hospitali ya mkoa Singida Musa Mohammed alisema kuwa wakiwa wanasubiri kuupakia mwili wa marehemu Gerald, lilitokea kwa kasi basi hilo na ghafla lilikwepa gari la polisi lililokuwa limesimama kuelekea basi linakotoka, kisha kuparamia kundi la watu na tangu hapo hakujielewa hadi alipozinduka asbuhi jana hospitalini. Alisema kuwa uchunguzi zaidi wa ajali hiyo unaendelea ili kujua chanzo halisi cha tukio pamoja na kumtafuta dereva wa basi la Sumry ili aweze kuhojiwa na kasha hatua za kisheria zeweze kuchukuliwa dhidi yake.

No comments:

Post a Comment