Tuesday 22 April 2014

WANANCHI WA VIJIJINI WATAKA WAJUMBE WA BUNGE LA KATIBA KUREJEA BUNGENI ILI WAENDELEE NA MCHAKATO WA KATIBA.

KAMANDA wa Umoja wa Vijana Jumuiya ya Chama Cha Mapinduzi(UVCCM) kata ya Gumanga Bw. Emmanuel Mkumbo akizawadia washindi mbalimbali wa soka baada ya mechi iliyozikutanisha timu ya Gumanga FC na Ikungu FC na Gumanga kkushinda 5-0 na kufanikiwa kujipatia jezi seti moja huku Ikungu ikijipatia mpira mmoja. Hiyo ilikuwa ni sehemu ya sherehe za kuapishwa kwake kuwa kamanda wa Jumuiya ya UVCCM Kata ya Gumanga.
KAMANDA wa Umoja wa Vijana Jumuiya ya Chama Cha Mapinduzi(UVCCM) kata ya Gumanga Bw. Emmanuel Mkumbo akiwa amebeba mkuki, pinde na mishale baada ya kuapishwa na mgeni rasmi katibu wa CCM Wilaya Mkalama Mkoani Singida Amosi Shimba kwenye uwanja wa mpira wa miguu wa shule ya sekondari Gumanga.
Na Elisante John, Mkalama Singida Aprili 22, 2014. BAADA ya wajumbe wa bunge la katiba kususia vikao vinavyoendelea mkoani Dodoma, wananchi wa maeneo ya vijijini katika wilaya ya Mkalama (Singida) wamewaomba wajumbe hao warejee haraka bungeni, ili waendelee kushiriki mchakato wa kupata katiba mpya. Wakiongea katika kijiji cha Gumanga juzi, wakati wa kumwapisha kamanda wa Umoja wa Vijana (UVCCM)Emmanuel Mkumbo wa kata ya Guamnga Wilaya Mkalama, baadhi ya wananchi hao John Peter, Grace Yindi na Fred Mabena wamewataka wajumbe hao kutanguliza mbele utaifa kwanza. Walisema kuwa badala ya kususia vikao vya bunge la katiba linaloendelea Mkoani Dodoma, sasa ni vyema wakarejea haraka bungeni, ili kuharakisha uundwaji wa katiba mpya ambayo itawakomboa Watanzania. "Kinachoendelea bungeni Dodoma siyo kitu kizuri, wao wanafanya mzaha na kuleta usimba na uyanga...waache mzaha, wafahamu kuwa sisi ndiyo tuliowatuma huko bungeni ili watutengenezee katiba ambayo itatufaa sisi Watanzania wote,"alisema John Peter wa Kijiji cha Maelu. Naye Grace Yindi mkazi wa Kijiji cha Kinankamba alisema kuwa uamuzi waliouchukua wa kutoka na kususia vikao vya bunge siyo njia sahihi ya kutatua kero na wala wasidhani kuwa jamii itawasikiliza kutokana na mgomo huo. Kutokana na hali hiyo Fred Mabena mkazi wa kijiji cha Guamanga aliwataka wajumbe hao wasione aibu kurejea bungeni badala yake wafanye haraka ili waendeleze mchakato wa kupata katiba mpya itakayokuwa na maslahi kwa Watanzania wote. Naye Mkumbo akizungumza baada ya kuapishwa kwake, aliwataka vijana kujiepusha na wanasiasa wenye lengo la kuchochea machafuko na hatimaye kusababisha vurugu hapa nchini. "Nchi hii ni yetu wote, nawaomba sana vijana wenzangu msikubali kuwasikiliza wala kutumiwa na watu wa aina hii wenye nia mbaya na nchi yetu...wao wanachotaka ni vurugu tu, achaneni nao na wala msiwasikilize," alisema Mkumbo. Hata hivyo mgeni rasmi kwenye hafla hiyo katibu wa CCM Wilaya ya Mkalama Amosi Shimba alimwomba kamanda huyo wa UVCCM kata ya Gumanga kuhakikisha anawatumikia vijana wote wa kata hiyo, bila kujali itikadi ya vyama vyao vya siasa. MWISHO.

No comments:

Post a Comment