Monday 7 April 2014

WANANCHI WA WILAYA YA IKUNGI WALALAMIKIWA KWA KUKOSA VYOO VYA KWA AJILI YA FAMILIA.

WASHIRIKI wa mafunzo ya usafi wa mazingira kutoka kata ya Puma katika halmashauri ya wilaya Ikungi Mkoani Singida wakimsikiliza kwa makini ofisa afya wa manispaa hiyo Richard Onesemo Rwehumbiza, yaliyoendeshwa na asasi ya Huruma Empowerment Foundation ya mjini Singida,kwa ufadhili Foundation for Civil Society la jijini Dar es Salaam kwa kamati za mazingira za kata. PICHA ya mwisho inamwonyesha mwezeshaji Onesmo Rwehumbiza akisisita jambo wakati akiwasilisha mada juu ya mbinu zinazostahili kutunza mazingira ili kuepukana na maradhi mablimbali.
Na Elisante John, Ikungi Aprili 07, 2014: USAFI wa mazingira ni suala muhimu hasa kwenye vyanzo vya maji na nyumbani kwa ajili ya kuweza kudhibiti magonjwa mbalimbali, yatokanayo na kinyesi cha binadamu na wanyama. Kama inavyoelezwa na Shirika la Afya Duniani (World Health Organisation), mamilioni ya watu waliopo kwenye nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania, hupoteza maisha yao kutokana na maradhi hayo, kuhara pia homa ya matumbo. Kutokana na hali hiyo asasi ya Huruma Empowerment Foundation ya mjini Singida, kupitia ufadhili wa Foundation for Civil Society la jijini Dar es Salaam imelaazimika kutoa mafunzo kwa kamati za mazingira za kata, katika Wilaya Ikungi, mkoani Singida. Mafunzo hayo yanatolewa na asasi ya Huruma Empowerment Foundation kwa kushirikiana na wataalamu wa afya wa wilaya hiyo na tayari vijiji vya kata ya Puma vimeanza kunufaika na mafunzo hayo. Lakini baada ya kukithiri kwa tatizo hilo kwa wananchi wa Wilaya Ikungi Mkoani Singida ambao hulazimika kujisaidia ovyo vichakani na porini, asasi hiyo inasema kero hiyo itakwisha iwapo jamii itakubali kubadilika kwa kiujenga vyoo bora. Richard Onesmo Rwehumbiza ni afisa afya Wilaya ya Ikungi mkoani Singida anasema zaidi ya asilimia 40 ya wananchi wa Wilaya hiyo sawa na kaya 22,000 bado wanajisaidia ovyo vichakani na porini kutokana na kukosa vyoo na kuvitumia. “Kwa kweli tatizo hili bado kubwa sana kwa jamii yetu…hii ni sawa na kuzalisha kinyesi kilo 11,000 kwa siku, ambacho ni sawasawa na uzito wa magari matatu ya Fuso kwa mwezi yenye uwezo wa kibeba mzigo tani tatu,”alifafanua kwa lugha rahisi Rwehumbiza. Wakati mtaalamu huyo akisema hayo Mwajuma Rajabu na Nicolous King’ale wote wakazi wa kijiji cha Kituntu kata ya Puma wanaikumbusha jamii kuongeza bidii ya usafi nyumbani, kwenye vyanzo vya maji na hata kwenye mashamba yao, ili kuepuka maradhi yanayotokana na uchafu. Aidha Christopher Lazaro wa kijiji cha Wibia alisema kuwa pamoja na kuwepo changamoto nyingi katika kukabiliana na kero ya uchafuzi wa mazingira, pia anahimiza suala la upandaji miti na jamii kupatiwa elimu ya kutosha juu ya mazingira ili wawe na maarifa ya kutosha kukabili tatizo hilo. Hata hivyo mratibu wa asasi ya Huruma Empowerment Christopher Lazaro Kwa mujibu wa Mratibu wa asasi ya Huruma Empowerment Christopher Yoeli Sungi, mafunzo hayo yatasaidia kuimarisha uwezo wa jamii vijijini kuweza kukabiliana na tatizo la usafi wa mazingira. MWISHO.

No comments:

Post a Comment