Monday 22 June 2015

BENKI YA NBC, TAWI LA SINGIDA YASAIDIA MASHUKA 30, KWA HOSPITALI YA MKOA WA SINGIDA.

MKUU wa Wilaya ya Singida, Saidi Amanzi (kulia), akikabidhi moja ya shuka kwa mganga mfawidhi, hospitali ya mkoa Singida,Dk.Ramadhani Kabala,kati ya mashuka 30 @ 15,000/=, baada ya mkuu wa wilaya huyo kupokea kutoka kwa meneja wa benki ya NBC Tawi la Singida, Japheth Mazumira, ili kupunguza uhaba wa mashuka na magodoro, kwenye hospitali hiyo.
KAIMU afisa Muuguzi mkuu, hospitali ya Mkoa wa Singida, Teresia Ntui (kushoto, mganga mfawidhi na watumishi wengine wa hospitali hiyo, wakifurahia pamoja, muda mfupi baada ya kupokea msaada wa mashuka 30, kutoka kwa benki ya NBC, Tawi la Singida.
MENEJA benki ya NBC, Tawi la Singida, Japheth Mazumira (kushoto), akikabidhi shuka kwa mkuu wa wilaya Singida, Saidi Amanzi, kwa ajili ya kukabiliana na upungufu wa mashuka na magodoro katika hospitali hiyo. Wengine wanaoshuhudia ni wataalamu wa afya katika hospitali hiyo.
BAADHI ya wanawake waliojifungua wodi ya sita, katika hospitali hiyo,wakiwa wamekaa watatu kwenye kitanda kimoja, huku wameshikilia watoto wao, kutokana na uhaba mkubwa wa mashuka na magodoro.
Na Elisante John, Singida Juni 22, 2015. HOSPITALI ya Mkoa wa Singida inakabiliwa na upungufu mkubwa wa mashuka zidi ya 2,000 na magodoro 230, hali inayoathiri utoaji huduma ya afya na uzazi kwa wagonjwa na wajawazito wanaokwenda kupata tiba kwa afya na uzazi. Mkuu wa wilaya ya Singida, Saidi Amanzi, Mganga mafawidhi wa hospitali hiyo, Dk. Ramadhani Kabala na kaimu afisa muuguzi mkuu, Teresia Ntui, wametoa wito kwa wadau mbalimbali kusaidia vifaa mbalimbali, ikiwemo mashuka na magodoro, ili kuboresha hudumza ya afya. Ili kukabiliana na changamoto hizo, benki ya NBC, Tawi la Singida, imetoa msaada wa mashuka 30, kwa ajili ya kupunguza kero wanazokumbana nazo wagonjwa, katika hospitali hiyo. Hospitali ya Mkoa wa Singida iliyojengwa mwaka 1954, ina jumla ya vitanda 300, lakini hivi sasa serikali ya Mkoa inaendelea na ujenzi wa hospitali kubwa ya rufaa, katika eneo la Mandewa, manispaa ya Singida.

Monday 18 May 2015

MBUNGE VITI MAALUMU (CCM) MKOA WA SINGIDA ATOA MSAADA KWA JUMUIYA YA UWT NA VIKUNDI VYA VIJANA

Na Elisante John, Singida Mei 18, 2015. IKIWA imebakia miezi mitano, kabla ya Tanzania kufanya uchaguzi mkuu, Wanawake wametakiwa kujenga tabia ya kupendana na kuonyana kwa upendo, ili kupata viongozi bora. Hayo yameelezwa na mbunge viti maalumu Mkoa wa Singida, na mjumbe kamati ya siasa mkoa wa Singida, Martha Mlata, alipokuwa akiongea na wanawake wa Wilaya ya Mkalama, Iramba, Ikungi na Singida Mjini, waliokutana, ili kujitathimini, kabla ya uchaguzi mkuu, utakaofanyika Oktoba, mwaka huu. Licha na tathimini hiyo, Mlata pia alitoa msaada wa pikipiki saba kwa ajili ya jumuiya ya UWT Wilaya ya Mkalama, Iramba, Singida mjini, Singida vijijini na Ikungi, pia alikabidhi baiskeli kwa ajili ya makatibu kata UWT, katika kata zote za mkoa wa Singida. Pia alikabidhi pikipiki moja na jezi jozi nne kwa ajili ya kikundi cha vijana, kilichopo kwenye kijiji cha Ibaga, wilaya ya Mkalama.

Sunday 7 December 2014

BENKI YA NMB, TAWI LA SINGIDA IMESHEREHEKEA SIKU YA KUJUMUIKA NA WAFANYAKAZI WOTE, 'NMB FAMILY DAY', KWA AMANI, NA KUFANA KWA KIWANGO KIKUBWA, HUKU WAFANYAKAZI WAKE WAKILA, KUNYWA NA KUFURAHIA KUPITIA MICHEZO MBALIMBALI

SHEREHE KWA WAFANYAKAZI WA BENKI YA NMB, TAWI LA SINGIDA JINSI ZILIVYOFANA KATIKA VIWANJA VYA HOTELI YA KBH, ILIYOPO ZIWA SINGIDANI.
BENKI ya NMB, Tawi la Singida imefanya sherehe kubwa kwa ajili ya siku ya wafanyakazi wake, ‘NMB Family’, iliyofanyika katika hotel ya KBH mjini Singida na kufana kwa kiwango kikubwa. Licha ya familia hizo kukutana pamoja, pia yalifanyika mashindano mbalimbali, ikiwemo kufukuza kuku (wanaume na wanawake), mpira wa miguu (wanaume) na muziki (dansi) kwa watoto. Hata hivyo watoto wawili wa mtumishi wa benki hiyo, Bw. Joseph, walifanikiwa kushinda baada ya kusakata vyema muziki wa kizazi kipya na kupewa zawadi mbalimbali na meneja wa tawi hilo, Bibi.Christine Mwangomo. MWISHO

BENKI YA NMB, TAWI LA SINGIDA IMEKABIDHI WATEJA WAKE WAWILI ZAWADI YA BAISKELI, BAADA YA KUSHINDA SHINDANO LILILOANZISHWA NA BENKI HIYO KWA AJILI YA WATEJA WANAOWEKA FEDHA KUPITIA AKAUNTI ZAO, KWENYE BENKI HIYO

MENEJA wa benki ya NMB, Tawi la Singida Bibi. Christine Mwangomo (kulia, akimpa mkono wa hongera mmoja wa wateja kati ya wawili, walioshinda shindano na weka ushinde (mwingine aliyeshinda ni mwanamke lakini hayupo kwenye picha), baada ya kuweka fedha kwenye akaunti yake na kujishindia baiskeli mpya. katikati ni meneja msaidizi wa tawi hilo, Bw. Makoyi.

MBUNGE VITI MAALUMU (CCM) MKOA WA SINGIDA, MARTHA MLATA AMEISAIDIA SEKONDARI YA NDUGUTI SH.MILIONI TATU KUONDOA TATIZO LA MAJI SHULENI HAPO

MBUNGE viti maalumu (CCM) Mkoa wa Singida, Martha Mlata ametoa msaada wa shilingi milioni tatu kwa sekondari ya kata ya Nduguti, wilaya ya Mkalama mkoani Singida, kwa ajili kuodoa tatizo la maji linaloikabili shule hiyo kwa muda mrefu sasa. Alilazimika kutoa kiasi hicho, baada ya kusomwa risala kwenye mahafali ya sita ya shule hiyo, kwamba inakabiliwa na changamoto nyingi, mojawapo ikiwa ni tatizo la maji, ambalo husababisha wanafunzi kupoteza muda mwingi kusaka maji, badala ya kushiriki masomo. Hata hivyo Mlata aliitaka halmashauri ya wilaya ya Mkalama kuhakikisha nayo inachangia kiasi cha fedha kitakachopungua, ili kazi ya kuvuta maji kwa kutumia mtandao wa bomba iweze kukamilika haraka, na yeye akabidhiwe mapema januari mwakani wakati shule zitakapofunguliwa. Licha ya kutoa kiasi hicho cha fedha, Mlata alikabidhi pia mipira na jezi za mchezo wa soka, kwa ajili ya wasichana na wavulana wa shule hiyo, msaada uliogharimu zaidi ya Sh.laki mbili na nusu. MWISHO.

SERIKALI YA MKOA WA SINGIDA IMETAKIWA KUMALIZA HARAKA MIGOGORO YA MIPAKA ILI KUWEZESHA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA HAPO DISEMBA 14, 2014, KUFANYIKA KWA AMANI

Na Elisante John, Singida SERIKALI imetakiwa kutatua migogoro ya mipaka, ili kufanikisha zoezi la uchaguzi wa serikali za mitaa, utakaofanyika disemba 14, 2014. Rai hiyo imetolewa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida, kupitia mwenyekiti Mgana Msindai na katibu wake Mary Chatanda, wakati wa kikao cha kamati ya ushauri cha Mkoa. “Mheshimiwa mwenyekiti, iwapo tatizo hili litaondolewa, nina uhakika wananchi wetu watashiriki vyema zoezi la uchaguzi wa serikali ya mitaa, utakaofanyika hivi karibuni,”alisema Chatanda. Msindai alibainisha kuwa, tatizo hilo limekithiri mkoani Singida, kuanzia ngazi ya kitongoji, vijiji, kata, wilaya, pia kati ya mkoa wa Singida na baadhi ya majirani zake, ikiwemo wilaya ya Uyui, mkoani Tabora. Aliiomba serikali kumaliza haraka tatizo hili, ili wananchi waweze kushiriki vyema uchaguzi wa serikali za mitaa, ambao baadhi ya wananchi wapo hatarini kupiga kura, kutokana na kukithiri kwa migogoro hiyo. Aidha mbunge viti maalumu (CCM) Mkoa Singida, Mathar Mlata aliomba fedha za upimaji ardhi zinapopatikana kwa kila halmashauri, zikafanye kazi katika maeneo ya vijiji, badala ya kuanza na makao makuu ya wilaya. Makamu mwenyekiti halmashauri wilaya Singida, Elia Digha aliitaka serikali kutatua mgogoro wa mpaka, kati ya manispaa Singida na wilaya yake, katika eneo la Njiapanda, ambako kuna mnada maarufu, kila siku ya jumamosi. Akijibu hoja hiyo, katibu tawala mkoa Singida, Liana Hassan alisema serikali inatambua tatizo hilo, akawaomba wajumbe kuvumilia wakati huu, ambao jitihada zinafanyika, ili kutatua kero hiyo. “Tatizo hili limekuwa likishughulikiwa kwa muda sasa…nawaomba sana wajumbe muendelee kuwa wavumilivu, baada ya uchaguzi utatuzi wa migogoro hii itakuwa imepatiwa ufumbuzi,”alisema. Akihitimisha, mkkuu wa mkoa wa Singida, Dk. Parseko Kone aliagiza wakuu wa wilaya na sekretarieti ya mkoa kumaliza tatizo hilo haraka, pia mgogoro wa mpaka kati ya wilaya za Manyoni (Singida) na Sikonge (Tabora). MWISHO.

Sunday 11 May 2014

ELIMU INAWEZA KUMKOMBOA BINADAMU, HASA KAMA ATAZINGATIA IPASAVYO MASOMO YAKE. JULIUS CHARLES NI MWANAFUNZI WA DARASA LA SITA ANAYETUMIA MGUU WAKE WA KULIA KUANDIKA DARASANI KUTOKANA NA ULEMAVU ALIONAO WA MIKONO.

WANAFUNZI wa Shule ya Msingi Ikungi Mchanganyiko, kitengo cha walemavu (wasioona) wakiwa darasani kuendelea na masomo chini ya walimu wao.
MWANAFUNZI Julius Charles mlemavu wa mikono, akiwa darasani huku akiandika kwenye daftari lake kwa kutumia vidole vya mguu wake wa kulia.
Julius akitandika kitanda chake kwa kutumia mguu wake wa kulia.
Akiwa kwenye darasa la kawaida (mbele aliyeweka daftari chini huku akiandika),pamoja na wanafunzi wenzake wasiokuwa na ulemavu.
Julius akitoka darasanibaada ya kumaliza kipindi na wanafunzi wenzake wasiokuwa na ulemavu.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Olvary Kamilly akiwa ofisini kwake, akizungumza na mwandishi wa habari hizi (hayupo pichani), alisema jamii ya walemavu inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo wazazi kuwaficha majumbani, pia kuwahudumia watu wa aina hii ni gharama kubwa na akaiomba jamii kuisaidia shule hiyo kwa hali na mali.
Singida. Mei 12, 2014. KUNA methali isemayo ‘Shida huleta maarifa’ na ‘Kama hujafa hujaumbika.Julius Charles (12) ni mlemavu wa viungo, anayesoma shule ya msingi Ikungi mchanganyiko, iliyopo Wilaya Ikungi, Mkoani Singida. Ni mlemavu wa mikono, lakini kutokana na bidii darasani ameweza kumudu vyema kusoma na kuandika, hali inayomwezesha awazidi hata wenzake wazima anaosoma nao darasa la sita. Alianza elimu ya msingi mwaka 2006 kwa msaada wa mama yake aliyepata taarifa juu ya shule hiyo yenye kuchukua wanafunzi Mchanganyiko (yaani wenye afya njema) na walemavu ambao wanaishi bweni. Julius alizaliwa kijiji cha Mgungari Wilaya Bunda mkoani Mara mwaka 2002, ni mtoto wa kwanza wa bwana na bibi Charle Namwanga, lakini baba yake aliugua ugonjwa wa akili, hivyo kumtegemea zaidi mama yake, serikali na wahisani kupata mahitaji muhimu. Anamudu vyema masomo yake kutokana na ushirikiano wa walimu tangu akiwa darasa la kwanza, na sasa wenzake na walimu humsaidia kwa kukamatisha kalamu kwenye mguu wa kulia, naye huandika vyema hata kuwazidi wengine wenye mikono kamili. Licha ya kufanya vyema darasani na kushika nafasi ya tatu kati ya wanafunzi 62, Julius pia humudu kuoga na kufanya kazi nyinginezo ndogondogo, ikiwemo kutandika kitanda, lakini anatoa somo kwa walemavu kujiendeleza kimasomo ili baadaye wajikomboe kiuchumi. Kama walivyo watu wengine wenye malengo ya baadaye, ndoto ya Julius ni kuwa mwanasiasa aliyebobea, ili aweze kuwasemea walemavu wenzake akiwa bungeni. Olivary Kamilly ni mwalimu mkuu wa shule hiyo, anasema Julius ni mwanafunzi anayezingatia masomo na hushiriki madarasa yote mawili, akianza na la kawaida, kisha baadaye darasa la walemavu, ingawa pia changamoto zipo nyingi zinazoikabili shule hiyo. Mwalimu Kamilly anaiomba jamii kuacha kuwatenga watoto wenye ulemavu, badala yake wawathamini na wajitahidi kuwasomesha katika shule maalumu, ili baadaye waweze kukidhi matarajio yao. Pia ameiomba jamii kuisaidia shule hiyo ili iweze kumudu vyema kuwahudumia wanafunzi wenye matatizo ya ulemavu. Adamu Bilali ni mwalimu mlemavu wa macho na Anna Mjema ni mwalimu wa wanafunzi wenye ulemavu katika shule hiyo, wanasema kuwa jamii hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo ugumu wa kufundisha mlemavu kama huyu. MWISHO.