Saturday 28 September 2013

MWANAMKE ATUHUMIWA KUMUUA MJUKUU WAKE WA KIKE..

MAELEZO YA PICHA:Mwenyekiti Mtaa wa Lulumba New Kiomboi katika wilaya Iramba Bw. Abel Seith akizungumza na wanahabari (hawapo pichani) juu ya kifo cha msichana Zuhura Alfred (6) kumwagiwa maji ya moto na mtu anayedaiwa kuwa bibi aliyetajwa kwa jina la Magreth Sombi (55) na kumsababishia mauti. PICHA YA MWANAMKE ALIYEFUNGA KICHWA KITAMBAA: Ni mtuhumiwa Magreth Sombi (55) anayedaiwa kuhusika na mauaji ya mjukuu wake (Zuhura) baada ya kummwagia maji ya moto aliyokuwa atumie kusongea ugali majira ya jioni. PICHA YA MSICHANA ALIYEVAA NYWELE BANDIA:Ni binti wa Magreth anayejulikana kwa jina la Naomi Sanga (20) anayedaiwa kushirikiana na mama yake mzazi katika mauaji ya mtoto Zuhura kwa kumwagia maji ya moto. Naomi amehitimu mafunzo ya ualimu mkoani Tabora hivi karibuni na anasubiri kupangiwa kituo cha kazi. Naomi na mama yake wanashikiliwa na Polisi wilayani Iramba juu ya mauaji hayo. Na Elisante John,Kiomboi-Iramba Septemba 28, 2013:MSICHANA aliyejulikana kwa jina moja la Zuhura Alfred (6) mkazi wa mtaa wa Lulumba-New Kiomboi wilaya Iramba mkoa wa Singida amefariki dunia kutokana na kile kilichoelezwa na wananchi kuwa kifo hicho kimetokana na kumwagiwa maji ya moto na bibi yake aliyetajwa kwa jina la Magreth Sombi (55). Mwanamke huyo alimmwagiwa motto maji hayo ambayo yalikuwa yatumike kusongea ugali majira ya jioni baada ya mtoto kuwa amechelewa kupeleka mwiko wa kupikia aliokuwa ametumwa kutoka kabatini. Akieleza kisa hicho Mwenyekiti wa mtaa huo Abel Seth Muna alisema tukio hilo lilitokea siku ya jumanne (septemba 24) mwaka huu majira ya jioni katika eneo wanaloishi, mtaa wa Lulumba-New Kiomboi. Alisema siku hiyo marehemu baada ya kuchelewa kuukabidhi mwiko huo kutoka alikotumwa, alimwagiwa maji ya moto yaliyokuwa yamechemka tayari kutumika kupikia ugali na kujeruhiwa vibaya katika sehemu kubwa ya mwili wake ikiwemo mikononi na miguuni kiasi cha nyama za mikononi kumomonyoka "Kama hiyo haikutosha, Magreth kwa kushirikiana na mwanae (Naomi) walimkamata kwa nguvu mtoto huyo na kutumbukiza viganja vyake vyote ndani ya sufuria lililokuwa na maji ya moto....mtoto aliungua sana hadi nyama zote za mkononi zikatoka...,"alisema kwa masikitiko. Mwenyekiti huyo alisema binti huyo alifariki dunia siku ya pili yake siku ya septemba 26 akipatiwa tiba katika hospitali ya wilaya ya Iramba, mjini Kiomboi. Alisema baada ya binti huyo kufariki Magreth alimtuma Naomi kwenda nyumbani kwa mwenyekiti kutoa taarifa juu ya kifo hicho huku akiacha kuwataarifu majirani zake waliomzunguka. "Nilipomhoji sababu ya kutowajulisha majirani zake, aliniomba nisiwaambie kwa sababu hataki watu wengi wajue au waje kurundikana kwake eti mwili wa Zuhura utachukuliwa na ndugu zake kwenda kuzika Singida mjini wakati wowote,"alisema kwa masikitiko Seth. Naye jirani mwingine wa karibu Elieza Mgwali alisema msichana huyo ambaye ana miezi miwili tangu aanze kuishi na bibi yake alikuwa na wakati mgumu kutokana na mateso aliyokuwa anapata kutoka kwa bibi yake (Magreth). "Mtoto ameteseka sana, alifanyishwa kazi nzito ambazo zipo nje ya uwezo wake na alikuwa ananyimwa mpaka chakula...alikuwa anakuja kwangu moja kwa moja anaingia jikoni kutafuta chakula, tulishatambua mateso yake hivyo tulikuwa tunamruhusu ale mpaka ashibe,"alisema Mgwali. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida Geofrey Kamwela amekiri kuwepo kwa tukio hilo na amesema kuwa tayari Naomi na mama yake (Magreth) wanashikiliwa, tayari kupandishwa kizimbani wakati wowote. MWISHO.

No comments:

Post a Comment