Sunday 30 March 2014

SHULE YA SEKONDARI UNYAHATI HAINA CHOO WALA MADAWATI.

BAADHI ya wanafunzi wa shule ya sekondari Unyahati iliyopo tarafa ya Ikungi Wilaya ya Ikungi mkoani Singida wakitumia viti vya plastiki kukalia na mapaja kukandamizia daftari wakati wa kuandika. Pia kwenye picha kinaonekana choo cha shimo kikiwa kimezungushiwa majani ya mimea jambo ambalo ni hata wakati wa masika, kwa mujibu wa mwalimu Mboya David wa shule hiyo shimo la choo hicho hutitia wakati wa mvua za masika na kulazimika kuchimba kingine wmajira ya kiangazi. Picha nyingine ikionyesha ofisi ya mkuu wa shule, ambacho kimetokana na moja ya darasa kutumika kama ofisi, hiyo yote imetokana na jamii inayozunguka shule hiyo kukataa kuchangia miradi ya maendeleo wakidai kuwa serikali inazo fedha za kutosha.
Na Elisante John, Ikungi March 30, 2014. SHULE ya sekondari Unyahati iliyopo wilaya ya Ikungi Mkoani Singida inakabiliwa na matatizo mbalimbali ikiwemo uhaba wa vyoo hali inayohatarisha afya kwa wanafunzi wanaolazimika kutumia choo cha nyasi. Kaimu mkuu wa shule hiyo Mboya David alisema kutokana na wazazi au walezi kutochangia miradi ya maaendeleo ikiwemo ile ya sekta ya elimu, walimu na wanafunzi wa shule hiyo walilazimika kuchimba choo hicho ambacho hata hivyo wakati wa masika hutumbukia ardhini. "Hapa kijijini ukizungumza juu ya michango!, wazazi na walezi hawatakuelewa, wameelezwa na viongozi wao kuwa serikali inazo fedha nyingi kwa jili ya kugharamia miradi yote…Wananchi hawahusiki kabisa na shughuli za kuchangia fedha,’alisema mwalimu huyo. Kufuatia kero hiyo, mwalimu David ameiomba serikali kuniusuru shule hiyo kwa kutenga fedha kwa ajili ya kukabiliana na kero mbalimbali ikiwemo ujenzi wa vyoo jambo ambalo ni muhimu sana kiafya. David alizitaja changamoto nyingine shuleni hapo ni wanafunzi wa kidato cha kwanza kutumia viti vya plastiki darasani, hali inayosababisha waweze kuandika wakiwa wanatumia mapaja yao kama meza. Changamoto nyingine shuleni hapo ni kukosekana kwa nyumba za walimu na kusababisha walimu kutembea kilomita nane kwenda na kurudi shuleni hai makao makuu ya Wilaya, mjini Ikungi walikopanga. "Jengo la utawala tunalotumia limetokana na kubadili matumizi ya vyumba viwili vya madarasa… tunakabiliwa na upungufu mkumbwa wa samani ikiwemo makabati kitendo kinachotulazimisha kutumia viti vya plasitiki kuhifadhia nyaraka mbalimbali,"alisema mwalimu David. Kuhusu vyumba vitatu vya maabara,David alisema kuwa hali ni mbaya mno kwa sababu hata kutenga eneo lenyewe la kujenga vyumba hivyo,halijatengwa. MWISHO.

Monday 24 March 2014

MKUTANO MKUU WA SINGIDA PRESS CLUB WAFANYIKA MANYONI KWA AMANI NA KUPATA KATIBU MTENDAJI MPYA.

VIONGOZI wa juu wa Klabu ya wanahabari Mkoa wa Singida, Mwenyekiti Seif Takaza (katikati), kushoto ni katibu msaidizi Emmanuel Michael na Damiano Mkumbo-Makamu mwenyekiti wakati wa mkutano mkuu uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano (Maktaba) mjini Manyoni.
SEHEMU ya wajumbe wa kamati ya utendaji Hudson Kazonta (kushoto) akiwa na mjumbe mwenzake wakifuatilia kwa makini maendeleo ya mkutano huo. Na Elisante John, Manyoni March 24,2014. KLABU ya wanahabari Mkoa wa Singida imefanya uchaguzi mdogo na kumchagua mwanachama wake Pascal Tantau awe katibu mtendaji wa Singpress ili kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Abby Nkungu aliyejiuzulu disemba 30 mwaka jana kwa madai ya kuzorota afya yake. Katika mkutano mkuu huo wa mwaka uliofanyika kwa amani na utulivu Wilayani Manyoni, Pascal ambaye ni mwandishi wa kujitegemea gazeti la Raiatanzania, Tanzania daima na kituo cha Redio WAPO jijini Dar es Salaam, alipata kura 15 za ndio, mbili za hapana na kura moja iliharibika. Kutokana na uchaguzi huo mdogo uliofanyika wakati wa mkutano mkuu wa mwaka, Pascal atakuwa madarakani kwa mwaka mmoja hadi mwaka 2015 utakapofanyika uchaguzi wa viongozi wote ili kuendana sawa na mwongozo wa katiba ya Umoja wa klabu za waandishi wa habari nchini (UTPC). Akishukuru baada ya kuchaguliwa, Pascal aliwashukuru wanachama wote kwa kumwamini na kumpatia madaraka hayo makubwa na akaahidi kutumia nguvu, akili na uwezo wake wote kuisaidia klabu ili iweze kupiga hatua kubwa ya maendeleo. Kwa upande wake mwenyekiti wa klabu hiyo Seif Takaza aliwashukuru wanachama wote kwa kufanikisha kazi hiyo na akaongeza kuwa hii inaonyesha jinsi gani sasa klabu ilivyokomaa kutokana na wanachama pia uongozi bora chini ya usimamizi wa kamati ya utendaji ya Singpress. Uchaguzi huo ulilazimika kufanyika kufuatia aliyekuwa katibu wake Abby Nkungu kujiuzulu kwa madai kuwa ameagizwa na daktari wake anayeishi Nairobi nchini Kenya kwamba asifanye kazi inayomlazimu kutumia akili nyingi, kutokana na upasuaji wa jicho aliofanyiwa miaka mitano iliyopita. MWISHO.

Sunday 23 March 2014

JUMUIYA YA SERIKALI ZA MITAA (ALAT) na nchi ya CANADA ZAENDESHA MAFUNZO SINGIDA

KATIKA picha baadhi ya washiriki wa mafunzo wakisikiza kwa makini hotuba ya ufunguzi wa mafunzo uliofanywa na mkuu wa Wilaya Singida Mwalimu Queen Mlozi kwa ajili ya wataalamu wa halmashauri za wilaya, wenyeviti wa halmashauri na mameya wa Manispaa wa kanda ya kati (Singida, Tabora, Dodoma na Kigoma), yaliyofanyika ukumbi wa halmashauri Wilaya Singida, kwa ajili ya kuwaongezea uwezo wa kufanya kazi kwa weledi zaidi. Na Elisante John, Singida March 23, 2014:JUMUIYA ya Serikali za Mitaa (ALAT) kwa kushirikiana na serikali ya Canada, inaendesha mafunzo kwa wataalamu wa halmashauri za Wilaya, Miji, Manispaa na Majiji nchini ili kuwaongezea uwezo waweze kutekeleza majukumu yao kwa weledi. Hayo yalibainishwa juzi na Armstrong Amani,mratibu wa taifa mpango wa MPED, unaofadhili mafunzo hayo ambayo tayari yametolewa katika mikoa ya kanda ya ziwa, mashariki, kaskazini na sasa Mkoani Singida kwa kushirikisha mikoa ya Kigoma, Tabora, Dodoma na Singida. Armstrong alisema kuwa baada ya wataalamu wa halmashauri kupata mafunzo hayo, wataongeza ufanisi kazini kulingana na ubunifu watakaogundua kutokana na elimu wanayopatiwa kupitia mpango huo wa Municipal Partnership for Economic Development (MPED). Mapema akifungua mafunzo hayo, Mkuu wa Wilaya Singida Mwalimu Queen Mlozi aliwataka wataalamu hao kuhakikisha wanazingatia vyema mafunzo wanayofundishwa, ili baadaye siku za usoni yawasaidie kuwaleleta wananchi maendeleo. “Ninawaomba sana muwe makini muda wote wakati mnafundishwa…mkirudi lazima mkalete mabadiliko katika wilaya zenu ili wananchi wapate maendeleo kama vile ilivyokusudiwa na serikali,”alisema Mlozi. Aidha mwezeshaji wa mafunzo hayo Amosi Migire, ambaye pia ni mratibu kiongozi mpango wa MPED Mkoa Morogoro alisema kuwa mafunzo hayo yatakuwa chachu kubwa ya maendeleo katika halmashauri za wilaya nchini kutokana na kutumia dira na vipaombele vilivyowekwa kwenye maeneo husika. Kwa mujibu wa Amstrong, mpango wa Municipal Partnership for Economic Development duniani upo nchi za Tanzania, Bukinafaso, Mali, Cambodia, Nicaragua, Vietinam na Bolvia, huku katika bara kla Afrika ukihusisha nchi tatu pekee. Hapa nchini MPED unatoa mafunzo kwa maofisa maendeleo ya jamii, mipango, fedha, ushirika, maofisa biashara, madiwani (mwenyekiti au meya) na wakurugenzi wa halmashauri za wilaya. MAELEZO YA PICHA YA KWANZA-IMG 1387:Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya MPED kwa ajili ya kujengea uwemo, wakiwemo wataalamu,Wenyeviti na mameya wa halmashauri za wilaya na manispaa wa mikoa ya Kigoma, Tabora, Dodoma na Singida, yanayotolewa mjini Singida chini ya usimamizi wa mamlaka za serikali za mitaa nchini (ALAT) inayoshirikiana na nchi ya Canada. MAELEZO YA PICHA YA PILI IMG 1892:Mkuu wa Wilaya Singida Mwl. Queen Mlozi akifungua mafunzo hayo. PICHA na Elisante John-Singida. MWISHO.

MAKADA CCM WAIOMBA SERIKALI KUWADHIBITI WANASIASA WANAOZUIA JAMII KUCHANGIA MIRADI YA MAENDELEO

Picha mbalimbali zikionnyesha sherehe ya kuwaapisha Makamanda wapya wa CCM kutoka kata 26 za Wilaya Ikungi katika sherehe zilizofanyika Kijiji cha Makiungu, kata ya Mungaa mheni rasmi akiwa ni Mkuu wa Wilaya hiyo Manju Msambya.
Elisante John, Singida March 23, 2014. SERIKALI imeombwa kutumia nguvu ili kuwadhibiti wanasiasa wanaokwamisha Wananchi kuchangia fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye maeneo yao, hasa ile inayohusiana na sekta ya elimu. Hayo yamebainishwa na makada 26 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM0 walioapishwa na Mkuu wa Wilaya Ikungi mkoani Singida Manju Msambya kuwa makamanda wa chama hicho ngazi ya kata. Mmoja wa makada wa chama hicho Celestne Yunde alisema miradi mingi ya kijamii kwenye maeneo yanayoshikiliwa na vyama vya upinzani wilayani humo hivi sasa yapo nyuma kimaendeleo kutokana na viongozi wa vyama vya upinzani kuwakataza wananchi kuchangia fedha za miradi. Kutokana nna hali hiyo Yunde ambaye pia ni mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya Ikungi (CCM) aliiomba serikali kuwadhibiti wanasiasa wa aina hiyo, ili kuharakisha maendeleo kwenye maeneo hayo. Aidha Sanka Pius Sanka na alhaji Haji Mukhandi kutoka jimbo la Singida Mashariki walitoa wito kwa jamii kutowachagua tena wanasiasa wa aina hiyo wakati wa uchaguzi mkuu ujao, kutokana na kukwamisha maendeleo katika maeneo wanayoongoza. Walisema kuwa miaka mitano iliyopita jimbo hilo lilipiga hatua kubwa kwa ujenzi wa shule za sekondari baada ya kila kata kufanikisha zoezi hilo, lakini miaka minne baadaye ari ya jamii kuchangia maendeleo imeshuka, kiasi cha kusababisha kuwa jimbo la mwisho Singida katika ujenzi wa vyumba vya maabara. “Kuingia madarakani kunahitaji mbinu nyingi ili kuwashahwishi wananchi wakuchague kama wanavyofanya wanasiasa uchwara…wananchi sasa wamejifunza katika miaka hii minne, naamini hawatafanya kosa tena la kumchagua mtu anayewafaa kuwasaidia kuleta maendeleo,”alisema Sanka Pius. Kwa upande wake mgeni rasmi wakati wa kuwaapisha makamanda wapya wa CCM, Wilaya Ikungi Mkuu wa Wilaya hiyo Manju Msambya alisema kuwa kabla hajashughulikiwa na Serikali katika kutekeleza ujenzi wa vyumba vya maabara, atahakikisha anawashughulikia kwanza watu hao ili kukomesha tabia hiyo. “Ninachoweza kusema kwa watu kama hawa…mimi nilikula kiapo mbele ya mkuu wangu wa kazi mkuu wa mkoa, sitakubali kushughulikiwa kwa uzembe wa kushindwa kukamilisha ujenzi wa maabara, nitahakikisha nawashughulikia kwanza wote wanaokwamisha kazi hii,”alisema Mkuu huyo wa wilaya. Kwa mujibu wa Msambya, Wilaya hiyo ina jumla ya shule za sekondari 28, lakini hadi sasa maendeleo ya ujenzi wa vyumba vya maabra ni dhaifu kwa asilimia 18 mpaka 65, huku wilaya hiyo ikishika nafasi ya mwisho, wakati muda uliowekwa na Mkoa kukamilisha kazi hiyo ni juni 30 mwaka huu. Kwa mujibu wa Msambya wilaya zinazoongoza kwa ujenzi wa maabara mkoani Singida ni halmashauri ya wilaya Mkalama na Iramba. MWISHO.

WAUMINI WA KANISA LA WANDIVENTISTA (WASABATO) WAJITOLEA DAMU

Singida March 23, 2014. WAUMINI wa madhehebu mbalimbali ya dini na jamii kwa ujumla wametakiwa kujenga utamaduni wa kuchangia damu, ili kurahisisha upatikanaji wa damu salama kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa waliolazwa hospitalini. wanaohitaji waliolazwa hospitalini kutokana na kusumbuliwa na maradhi mbalimbali, ikiwemo pia wanaopatwa na ajali. Rai hiyo imtolewa na waumini wa kanisa la Waadiventista-WASABATO, lililopo Unyankindi mjini Singida, wakati wanachangia damu, chini ya usimamizi wa chama cha Msalaba mwekundu, Mkoa wa Singida. Walisema licha ya kuwasaidia wagonjwa wanaoteseka hospitalini kwa kupungukiwa damu, zoezi hilo pia linazidisha upendo miongoni mwao. Aidha Mkurugenzi wa vijana kutoka kanisa hilo Eliphasi Nkuka alisema upungufu wa damu uliopo katika hospitali nyingi nchini utakwisha na maisha ya wagonjwa wanaokabiliwa na tatizo hilo yataokolewa iwapo kutakuwa na akiba ya kutosha kwenye benki ya damu salama nchini. “Kazi hii ya kumponya binadamu ilianzishwa na Yesu mwenyewe…sisi tumeamua kujitolea kutoa damu ili kuwaokoa wenzetu wanaoteseka hospitalini kwa magonjwa mbalimbali na ajali..,”alisema mkurugenzi wa vijana katika kanisa hilo Eliphas Nguka. Zoezi hilo ililotanguliwa na msaada kwa wagonjwa waliolazwa hospitali ya Mkoa wa Singida mwingine uliopelekwa kituo cha watoto yatima Upendo kilichopo Manguamitogho Manispaa Singida , uligharimu zaidi ya Sh. 800,000. Naye mratibu wa Mkoa, mpango wa taifa damu salama Sostenes Ndyetabura aliitaka jamii kuiga mfano wa waumini wa kanisa la Wasabato ili kukabiliana na tatizo la upungufu wa damu lililopo katika akiba ya benki ya damu salama, ambayo kwa mkoa wa Singida, ipo Mkoani Tabora. Aidha muuguzi wa zamu wodi ya watoto hospitali ya Mkoa wa Singida Marieta Bayo kwa niaba ya watoto waliolazwa, alishukuru kwa msaada huo na kuomba msaada zaidi kutoka kwa wote wenye uchungu na watoto wanaoteseka hospitalini kutokana na maradhi mbalimbali. MWISHO.