Tuesday 29 April 2014

BASI LA KAMPUNI YA SUMRY LAPARAMIA NA KUUA WATU 19 WAKIWEMO ASKARI POLISI WANNE WALIKOKUWA KAZINI.

PICHA ZA Miili ya askari polisi wanne wa mkoa wa Singida, Boniface Magubika, Novatus Tarimo, Michael Mwakihaba na Jumanne Mwakihaba, ikiwa kwenye masanduku kwa ajili ya ibada ya kuagwa na mamia ya wakazi wa mji wa Singida kwenye viwanja vya line Polisi, tayari kwa kusafirishwa jana jioni kwenda kuzikwa katika mikoa yao walikozaliwa ikiwemo Kilimanjaro, Pwani, Iringa na Mbeya.
Na Elisante John, Singida Aprili 29, 2014. WATU 19 wamekufa, wakiwemo askari polisi wanne na wengine nane wamejeruhiwa vibaya baada ya kugongwa na basi la lililokuwa linatokea Mkoani Kigoma, kwenye eneo la kijiji cha Utaho Kata ya Puma Wilayani Ikungi, barabara kuu ya Sindida- Dodoma kilomita 15 kutoka Singida Mjini. Ajali hiyo ilitokea juzi usiku saa 2.45 na kulihusisha basi namba T 799 BET Nissan mali ya Kampuni ya Sumry, likitokea Kigoma kwenda jijini Dar es Salaam, likiendeshwa na Paulo Njilo mkazi wa jijini Dar es Salaam. Kamanda wa polisi Mkoa Singida Geofrey Kamwela alisema siku ya tukio hilo wananchi wakiwa na askari polisi wa doria walikuwa wamekusanyika pembezoni mwa barabara kuupakia mwili ya mtu mmoja mwendesha baiskeli aliyegongwa na lori na kufariki dunia. Alisema kuwa wakiwa katika harakati za kuupakia mwili huo kwenye gari la polisi namba PT 1424 huku likiwa limeegeshwa pembeni mwa barabara, gafla basi hilo lilikuja kwa kasi na kuwagonga wananchi hao na 15 dunia papo hapo, huku wengine watatu wakifariki dunia wakati wakipelekwa hospitalini. Akielezea tukio hilo, Kamwela alisema dereva wa basi baada ya kukaribia eneo hilo aliliona gari la polisi likiwa limepaki pembeni kushoto mwa barabara, lakini katika kulikwepa ndipo alipoparamia kundi la watu waliokuwa pamoja na askari na kuwagonga huku wengine wakipotez amaisha. Aidha alisema dereva wa basi hilo baada ya ajali hiyo aliendelea na mwendo hadi aliposimama kilomita 25 katika makao makuu ya wilaya Ikungi na kutokomea kusikojulikana, lakini juhudi za kumtafuta zinaendelea. Aliwataja askari waliokufa kuwa ni F.849 D/CPL Boniface Magubika wa CID Wilaya ya Singida, F.6837 Pc Jumanne Mwakihaba wa FFU Singida, G.7993 Pc, Novatus Tarimo wa ofisi ya RCO na G.8948 Pc, Michael Mwakihaba wa FFU Singida. Wengine waliokufa aliwataja kuwa ni afisa mtendaji kijiji cha Utaho Ramadhan Mjengi, Mwenyekiti wa kijiji Utaho Paul Hamis, Mwenyekiti wa kitongoji cha Utaho Ernet Salanga, Said Rajab, Usirika Itambu, Chima Mughenyi, Salim Juma, Abeid Ramadhan, Mwinyi Hamis, na Issa Hussein wote wakazi wa kijiji cha Utaho. Kamanda Kamwela alisema miili ya marehemu wengine wanne bado haijatambuliwa na ndugu zao na imehifadhiwa kwenye chumba cha maiti hospitali ya mkoa wa singida. Alisema majeruhi wawili wamelazwa katika hospitali ya Mkoa Singida na wengine sita wapo hospitali ya misheni Malikia wa Ulimwengu iliyopo Puma. Aidha miili ya askari polisi wote inatarajiwa kusafirishwa kwenda katika mikoa wanakotoka wakati wowote mara taratibu za kipolisi zitakapokamilika, ikiwa ni baada ya kuwasiliana na ndugu zao wa Rombo-Kilimanjaro, Pwani, Mbalizi Mbeya na Iringa. Akielezea ajali hiyo Kamanda Kamwela alisema awali majira ya sa 1:30 usiku ilitokea ajali ya mtembea kwa miguu Gerad Zefania aliyegongwa na lori na kufa papo hapo. Mmoja wa majeruhi aliyelazwa hospitali ya mkoa Singida Musa Mohammed alisema kuwa wakiwa wanasubiri kuupakia mwili wa marehemu Gerald, lilitokea kwa kasi basi hilo na ghafla lilikwepa gari la polisi lililokuwa limesimama kuelekea basi linakotoka, kisha kuparamia kundi la watu na tangu hapo hakujielewa hadi alipozinduka asbuhi jana hospitalini. Alisema kuwa uchunguzi zaidi wa ajali hiyo unaendelea ili kujua chanzo halisi cha tukio pamoja na kumtafuta dereva wa basi la Sumry ili aweze kuhojiwa na kasha hatua za kisheria zeweze kuchukuliwa dhidi yake.

Tuesday 22 April 2014

WANANCHI WA VIJIJINI WATAKA WAJUMBE WA BUNGE LA KATIBA KUREJEA BUNGENI ILI WAENDELEE NA MCHAKATO WA KATIBA.

KAMANDA wa Umoja wa Vijana Jumuiya ya Chama Cha Mapinduzi(UVCCM) kata ya Gumanga Bw. Emmanuel Mkumbo akizawadia washindi mbalimbali wa soka baada ya mechi iliyozikutanisha timu ya Gumanga FC na Ikungu FC na Gumanga kkushinda 5-0 na kufanikiwa kujipatia jezi seti moja huku Ikungu ikijipatia mpira mmoja. Hiyo ilikuwa ni sehemu ya sherehe za kuapishwa kwake kuwa kamanda wa Jumuiya ya UVCCM Kata ya Gumanga.
KAMANDA wa Umoja wa Vijana Jumuiya ya Chama Cha Mapinduzi(UVCCM) kata ya Gumanga Bw. Emmanuel Mkumbo akiwa amebeba mkuki, pinde na mishale baada ya kuapishwa na mgeni rasmi katibu wa CCM Wilaya Mkalama Mkoani Singida Amosi Shimba kwenye uwanja wa mpira wa miguu wa shule ya sekondari Gumanga.
Na Elisante John, Mkalama Singida Aprili 22, 2014. BAADA ya wajumbe wa bunge la katiba kususia vikao vinavyoendelea mkoani Dodoma, wananchi wa maeneo ya vijijini katika wilaya ya Mkalama (Singida) wamewaomba wajumbe hao warejee haraka bungeni, ili waendelee kushiriki mchakato wa kupata katiba mpya. Wakiongea katika kijiji cha Gumanga juzi, wakati wa kumwapisha kamanda wa Umoja wa Vijana (UVCCM)Emmanuel Mkumbo wa kata ya Guamnga Wilaya Mkalama, baadhi ya wananchi hao John Peter, Grace Yindi na Fred Mabena wamewataka wajumbe hao kutanguliza mbele utaifa kwanza. Walisema kuwa badala ya kususia vikao vya bunge la katiba linaloendelea Mkoani Dodoma, sasa ni vyema wakarejea haraka bungeni, ili kuharakisha uundwaji wa katiba mpya ambayo itawakomboa Watanzania. "Kinachoendelea bungeni Dodoma siyo kitu kizuri, wao wanafanya mzaha na kuleta usimba na uyanga...waache mzaha, wafahamu kuwa sisi ndiyo tuliowatuma huko bungeni ili watutengenezee katiba ambayo itatufaa sisi Watanzania wote,"alisema John Peter wa Kijiji cha Maelu. Naye Grace Yindi mkazi wa Kijiji cha Kinankamba alisema kuwa uamuzi waliouchukua wa kutoka na kususia vikao vya bunge siyo njia sahihi ya kutatua kero na wala wasidhani kuwa jamii itawasikiliza kutokana na mgomo huo. Kutokana na hali hiyo Fred Mabena mkazi wa kijiji cha Guamanga aliwataka wajumbe hao wasione aibu kurejea bungeni badala yake wafanye haraka ili waendeleze mchakato wa kupata katiba mpya itakayokuwa na maslahi kwa Watanzania wote. Naye Mkumbo akizungumza baada ya kuapishwa kwake, aliwataka vijana kujiepusha na wanasiasa wenye lengo la kuchochea machafuko na hatimaye kusababisha vurugu hapa nchini. "Nchi hii ni yetu wote, nawaomba sana vijana wenzangu msikubali kuwasikiliza wala kutumiwa na watu wa aina hii wenye nia mbaya na nchi yetu...wao wanachotaka ni vurugu tu, achaneni nao na wala msiwasikilize," alisema Mkumbo. Hata hivyo mgeni rasmi kwenye hafla hiyo katibu wa CCM Wilaya ya Mkalama Amosi Shimba alimwomba kamanda huyo wa UVCCM kata ya Gumanga kuhakikisha anawatumikia vijana wote wa kata hiyo, bila kujali itikadi ya vyama vyao vya siasa. MWISHO.

Tuesday 15 April 2014

MRADI WA UMEME UNAOTUMIA NGUVU YA UPEPO KUGHARIMU ZAIDI YA DOLA ZA KIMAREKANI MILIONI 285 SINGIDA.

NAIBU waziri wa nishati na mdini Stephen Maselle (kushoto) akisaini kitabu cha wageni katika eneo la uwezekezaji nishati ya umeme unaotumia nguvu ya jua unaotarajiwa kujengwa kwenye eneo la Kisaki chini ya kampuni ya Wind East unaofadhiliwa na nchi ya United Kingdom (UK), kulia kwake ni waziri wa nishati na mabadiliko ya hali ya hewa wa UK Gregory Barker, balozi wa UK hapa nchini Dianna Melrose, mkuu wa Mkoa Singida Dk. Prseko Kone (wa mwisho kushoto).
Wakiwa eneo la mradi lenye mkondo wa upepo mkali kwa ajili ya kuzalisha umeme unaotumia nguvu ya upepo. Na Elisante John, Singida Aprili, 2014. SERIKALI ya Uingereza imeiomba Tanzania kuharakisha mchakato wa kuharakisha ujenzi wa kuzalisha umeme unaotumia nguvu ya upepo Mkoani Singida, ambao utahifadhi pia mazingira, ili kupunguza tatizo la nishati hiyo nchini. Waziri wa nchi, wizara ya nishati na mabadiliko ya hali ya hewa wa Uingereza Gregory Barker (Mbunge) amesema hayo, alipotembelea eneo la uwekezaji umeme wa upepo, katika eneo la Kisaki, Mjini Singida. Naye naibu waziri nishati na madini Stephen Masele amelikumbusha shirika la umeme nchini (TANESCO) kukamilisha haraka mazungumzo kati yao na mwekezaji wa mradi huo kampuni ya Wind East Africa inayotarajiwa kutumia dola za Kimarekani zaidi ya Milioni 285 hadi kukamilika. Aidha mhandisi wa mradi huo Baptiste Bargés alisema ingawa mchakato huo unasuasua kuanza, lakini utakapoanza utasaidia sana kuongeza uwezo wa TANESCO wakati utakapounganishwa kwenye gridi ya taifa, wakati Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk Parseko Kone alieleza kufurahishwa na wananchi wa eneo la kisaki katika kuukubali mradi huo ambao utaongeza sana nishati hiyo nchini. Kwa mujibu wa naibu waziri Masele, jumla ya megawati 2,700 hadi 3,000 zinatarajiwa kuzalishwa hadi ifikapo mwaka 2015, wakati kwa sasa ni megawati 1,500 tu, ndizo zinazozalishwa nchini. MWISHO.

MKUTANO MKUU WA WADAU WA MASHAURIANO MANISPAA YA SINGIDA JUU YA MASTER PLAN YA MJI HUO KWA MIAKA 20 IJAYO.

MADIWANI wa Manispaa ya Singida wakiwa kwenye picha ya pamoja na mkuu wa Mkoa wa Singida Dk. Parseko Kone (wa tatu kutoka kushoto mbele waliokaa), baada ya kufungua mkutano mkuu wa Master plan ya mji wa Singida kwa miaka 20 ijayo uliofanyika ukumbi wa chuo cha VETA Mjini Singida.
WENYEVITI wa mitaa Manispaa ya Singida wakiwa na mgeni rasmi Dk. Parseko Kone kwenye picha ya pamoja katika mkutano huo.
Hawa nao ni watendaji wa kata Manispaa ya Singida katika mkutano huo.
Meya wa Manispaa ya Singida Shekhe Salum MOhammed Mahami akishukuru baada ya ufunguzi wa mkutano huo uliofanywa na mkuu wa Mkoa wa Singida Dk. Parseko Kone.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk. Kone akifungua mkutano huo.
Maofisa kitendo cha mipango miji Manispaa Singida wakiwa kazini katika mkutano huo.
Mkurugenzi wa Manispaa Singida Joseph Mchina (mbele kulia) akiwa na wajumbe wengine wakisikiliza kwa makini mada iliyokuwa inatolewa kwenye mkutano huo.

Tuesday 8 April 2014

KILIMO KINAWEZA KUWAKOMBOA VIJANA IWAPO WATAAMUA KUJISHUGHULISHA.

VIONGOZI wa Umoja wa Vijana wa CCM Mkoa wa Dodoma wakiwa na viongozi wao wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa, wakikabidhi Pikipiki tano kwa wenzao wa Singida tayari kwa ajili ya kuendelea na mbio za uzalendo kitaifa, makabidhiano yaliyofanyika kijiji cha Lusilile Wilayani Manyoni.
k
NAIBU Katibu mkuu Jumuiya ya Umoja wa Vijana Chama Cha Mapinduzi Zanzibar Shaka Hamud Shaka (kulia aliyekingwa)akipeana mkono na mmiliki wa shamba la kampuni ya Singida agriculture Co Ltd Bw. Ali Mohammed lililopo kijiji cha Mkiwa Wilaya Ikungi aliyeajiri vijana zaidi ya 300 kwenye shamba hilo. Pia katika ziara hiyo naibu katibu mkuu aligawa kadi za UVCCM kwa vijana 300 wanaofanya kazi katika shamba hilo (mwenye kofia kulia ni Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Singida Martin Lissu). PICHA nyingine inamwonyesha kijana akichapa kazi ya kuchambua maharage mabichi baada ya kuvuna, tayari kwa ajili ya kujaza kwenye kreti ili kusafirishwa nje ya nchi ikiwemo barani Ulaya. PICHA nyingine inaonyesha mmiliki wa shamba hilo Bw. Ali Mohammed (kulia)akimwomnyesha mgeni rasmi (katikati) naibu katibu mkuu Jumuiya ya UVCCM Shaka Humud Sshaka aliyefanya ziara shambani hapo akiwa na msafara wa pikipiki za uzalendo kitaifa, kushoto ni mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Singida Martin Lissu. Na Elisante John, Ikungi KILIMO hai ni moja ya kazi ambazo vijana wengi hawataki kufanya, lakini pamoja na fursa hii nzuri hali ni tofauti kwa wawekezaji wa nje ambao wamekuwa wananufaika kiuchumi kutokana na mazao bora wanayolima na kuvuana. Naibu katibu mkuu Jumuiya ya Umoja wa Vijana Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Zanzibar Shaka Hamdu Shaka alisema hayo kwenye msafara wa mbio za uzalendo za pikipiki kitaifa, alipokuwa anaongea na vijana wanaofanya kazi shambani mwa mwekezaji, Singida Agriculture Co Ltd, lililopo Mkiwa wilaya Ikungi. Naye meneja mkuu wa Singida Agriculture Co Ltd Ali Mohammed anasema wakulima wengi nchini bado wanakabiliwa changamoto nyingi katika kuboresha mazao yao, hali aliyodai kuwa wanayo kazi kubwa kuhakikisha wanakabiliana kikamilifu na matatizo hayo. Baadhi ya vijana wanaofanya kazi shambani humo akiwemo Anita Ramadhani,Jasmin Paulo na Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Singida Martine Lisu, walieleza fursa mbalimbali kupitia kilimo na maeneo mengine, ambao walisema kuwa iwapo vijana watajikita katika kazi hizo ni wazi maisha yao yataboreka. Mbio za hizo za pikipiki kitaifa zilizinduliwa na Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohammed Shein Februari 22 mwaka huu, zikiwa na lengo la miaka 50 ya Muungano wa Tanzania, yenye kauli ‘Tanzania kwanza’. MWISHO.

Monday 7 April 2014

WANANCHI WA WILAYA YA IKUNGI WALALAMIKIWA KWA KUKOSA VYOO VYA KWA AJILI YA FAMILIA.

WASHIRIKI wa mafunzo ya usafi wa mazingira kutoka kata ya Puma katika halmashauri ya wilaya Ikungi Mkoani Singida wakimsikiliza kwa makini ofisa afya wa manispaa hiyo Richard Onesemo Rwehumbiza, yaliyoendeshwa na asasi ya Huruma Empowerment Foundation ya mjini Singida,kwa ufadhili Foundation for Civil Society la jijini Dar es Salaam kwa kamati za mazingira za kata. PICHA ya mwisho inamwonyesha mwezeshaji Onesmo Rwehumbiza akisisita jambo wakati akiwasilisha mada juu ya mbinu zinazostahili kutunza mazingira ili kuepukana na maradhi mablimbali.
Na Elisante John, Ikungi Aprili 07, 2014: USAFI wa mazingira ni suala muhimu hasa kwenye vyanzo vya maji na nyumbani kwa ajili ya kuweza kudhibiti magonjwa mbalimbali, yatokanayo na kinyesi cha binadamu na wanyama. Kama inavyoelezwa na Shirika la Afya Duniani (World Health Organisation), mamilioni ya watu waliopo kwenye nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania, hupoteza maisha yao kutokana na maradhi hayo, kuhara pia homa ya matumbo. Kutokana na hali hiyo asasi ya Huruma Empowerment Foundation ya mjini Singida, kupitia ufadhili wa Foundation for Civil Society la jijini Dar es Salaam imelaazimika kutoa mafunzo kwa kamati za mazingira za kata, katika Wilaya Ikungi, mkoani Singida. Mafunzo hayo yanatolewa na asasi ya Huruma Empowerment Foundation kwa kushirikiana na wataalamu wa afya wa wilaya hiyo na tayari vijiji vya kata ya Puma vimeanza kunufaika na mafunzo hayo. Lakini baada ya kukithiri kwa tatizo hilo kwa wananchi wa Wilaya Ikungi Mkoani Singida ambao hulazimika kujisaidia ovyo vichakani na porini, asasi hiyo inasema kero hiyo itakwisha iwapo jamii itakubali kubadilika kwa kiujenga vyoo bora. Richard Onesmo Rwehumbiza ni afisa afya Wilaya ya Ikungi mkoani Singida anasema zaidi ya asilimia 40 ya wananchi wa Wilaya hiyo sawa na kaya 22,000 bado wanajisaidia ovyo vichakani na porini kutokana na kukosa vyoo na kuvitumia. “Kwa kweli tatizo hili bado kubwa sana kwa jamii yetu…hii ni sawa na kuzalisha kinyesi kilo 11,000 kwa siku, ambacho ni sawasawa na uzito wa magari matatu ya Fuso kwa mwezi yenye uwezo wa kibeba mzigo tani tatu,”alifafanua kwa lugha rahisi Rwehumbiza. Wakati mtaalamu huyo akisema hayo Mwajuma Rajabu na Nicolous King’ale wote wakazi wa kijiji cha Kituntu kata ya Puma wanaikumbusha jamii kuongeza bidii ya usafi nyumbani, kwenye vyanzo vya maji na hata kwenye mashamba yao, ili kuepuka maradhi yanayotokana na uchafu. Aidha Christopher Lazaro wa kijiji cha Wibia alisema kuwa pamoja na kuwepo changamoto nyingi katika kukabiliana na kero ya uchafuzi wa mazingira, pia anahimiza suala la upandaji miti na jamii kupatiwa elimu ya kutosha juu ya mazingira ili wawe na maarifa ya kutosha kukabili tatizo hilo. Hata hivyo mratibu wa asasi ya Huruma Empowerment Christopher Lazaro Kwa mujibu wa Mratibu wa asasi ya Huruma Empowerment Christopher Yoeli Sungi, mafunzo hayo yatasaidia kuimarisha uwezo wa jamii vijijini kuweza kukabiliana na tatizo la usafi wa mazingira. MWISHO.