Sunday, 7 December 2014

BENKI YA NMB, TAWI LA SINGIDA IMESHEREHEKEA SIKU YA KUJUMUIKA NA WAFANYAKAZI WOTE, 'NMB FAMILY DAY', KWA AMANI, NA KUFANA KWA KIWANGO KIKUBWA, HUKU WAFANYAKAZI WAKE WAKILA, KUNYWA NA KUFURAHIA KUPITIA MICHEZO MBALIMBALI

SHEREHE KWA WAFANYAKAZI WA BENKI YA NMB, TAWI LA SINGIDA JINSI ZILIVYOFANA KATIKA VIWANJA VYA HOTELI YA KBH, ILIYOPO ZIWA SINGIDANI.
BENKI ya NMB, Tawi la Singida imefanya sherehe kubwa kwa ajili ya siku ya wafanyakazi wake, ‘NMB Family’, iliyofanyika katika hotel ya KBH mjini Singida na kufana kwa kiwango kikubwa. Licha ya familia hizo kukutana pamoja, pia yalifanyika mashindano mbalimbali, ikiwemo kufukuza kuku (wanaume na wanawake), mpira wa miguu (wanaume) na muziki (dansi) kwa watoto. Hata hivyo watoto wawili wa mtumishi wa benki hiyo, Bw. Joseph, walifanikiwa kushinda baada ya kusakata vyema muziki wa kizazi kipya na kupewa zawadi mbalimbali na meneja wa tawi hilo, Bibi.Christine Mwangomo. MWISHO

BENKI YA NMB, TAWI LA SINGIDA IMEKABIDHI WATEJA WAKE WAWILI ZAWADI YA BAISKELI, BAADA YA KUSHINDA SHINDANO LILILOANZISHWA NA BENKI HIYO KWA AJILI YA WATEJA WANAOWEKA FEDHA KUPITIA AKAUNTI ZAO, KWENYE BENKI HIYO

MENEJA wa benki ya NMB, Tawi la Singida Bibi. Christine Mwangomo (kulia, akimpa mkono wa hongera mmoja wa wateja kati ya wawili, walioshinda shindano na weka ushinde (mwingine aliyeshinda ni mwanamke lakini hayupo kwenye picha), baada ya kuweka fedha kwenye akaunti yake na kujishindia baiskeli mpya. katikati ni meneja msaidizi wa tawi hilo, Bw. Makoyi.

MBUNGE VITI MAALUMU (CCM) MKOA WA SINGIDA, MARTHA MLATA AMEISAIDIA SEKONDARI YA NDUGUTI SH.MILIONI TATU KUONDOA TATIZO LA MAJI SHULENI HAPO

MBUNGE viti maalumu (CCM) Mkoa wa Singida, Martha Mlata ametoa msaada wa shilingi milioni tatu kwa sekondari ya kata ya Nduguti, wilaya ya Mkalama mkoani Singida, kwa ajili kuodoa tatizo la maji linaloikabili shule hiyo kwa muda mrefu sasa. Alilazimika kutoa kiasi hicho, baada ya kusomwa risala kwenye mahafali ya sita ya shule hiyo, kwamba inakabiliwa na changamoto nyingi, mojawapo ikiwa ni tatizo la maji, ambalo husababisha wanafunzi kupoteza muda mwingi kusaka maji, badala ya kushiriki masomo. Hata hivyo Mlata aliitaka halmashauri ya wilaya ya Mkalama kuhakikisha nayo inachangia kiasi cha fedha kitakachopungua, ili kazi ya kuvuta maji kwa kutumia mtandao wa bomba iweze kukamilika haraka, na yeye akabidhiwe mapema januari mwakani wakati shule zitakapofunguliwa. Licha ya kutoa kiasi hicho cha fedha, Mlata alikabidhi pia mipira na jezi za mchezo wa soka, kwa ajili ya wasichana na wavulana wa shule hiyo, msaada uliogharimu zaidi ya Sh.laki mbili na nusu. MWISHO.

SERIKALI YA MKOA WA SINGIDA IMETAKIWA KUMALIZA HARAKA MIGOGORO YA MIPAKA ILI KUWEZESHA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA HAPO DISEMBA 14, 2014, KUFANYIKA KWA AMANI

Na Elisante John, Singida SERIKALI imetakiwa kutatua migogoro ya mipaka, ili kufanikisha zoezi la uchaguzi wa serikali za mitaa, utakaofanyika disemba 14, 2014. Rai hiyo imetolewa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida, kupitia mwenyekiti Mgana Msindai na katibu wake Mary Chatanda, wakati wa kikao cha kamati ya ushauri cha Mkoa. “Mheshimiwa mwenyekiti, iwapo tatizo hili litaondolewa, nina uhakika wananchi wetu watashiriki vyema zoezi la uchaguzi wa serikali ya mitaa, utakaofanyika hivi karibuni,”alisema Chatanda. Msindai alibainisha kuwa, tatizo hilo limekithiri mkoani Singida, kuanzia ngazi ya kitongoji, vijiji, kata, wilaya, pia kati ya mkoa wa Singida na baadhi ya majirani zake, ikiwemo wilaya ya Uyui, mkoani Tabora. Aliiomba serikali kumaliza haraka tatizo hili, ili wananchi waweze kushiriki vyema uchaguzi wa serikali za mitaa, ambao baadhi ya wananchi wapo hatarini kupiga kura, kutokana na kukithiri kwa migogoro hiyo. Aidha mbunge viti maalumu (CCM) Mkoa Singida, Mathar Mlata aliomba fedha za upimaji ardhi zinapopatikana kwa kila halmashauri, zikafanye kazi katika maeneo ya vijiji, badala ya kuanza na makao makuu ya wilaya. Makamu mwenyekiti halmashauri wilaya Singida, Elia Digha aliitaka serikali kutatua mgogoro wa mpaka, kati ya manispaa Singida na wilaya yake, katika eneo la Njiapanda, ambako kuna mnada maarufu, kila siku ya jumamosi. Akijibu hoja hiyo, katibu tawala mkoa Singida, Liana Hassan alisema serikali inatambua tatizo hilo, akawaomba wajumbe kuvumilia wakati huu, ambao jitihada zinafanyika, ili kutatua kero hiyo. “Tatizo hili limekuwa likishughulikiwa kwa muda sasa…nawaomba sana wajumbe muendelee kuwa wavumilivu, baada ya uchaguzi utatuzi wa migogoro hii itakuwa imepatiwa ufumbuzi,”alisema. Akihitimisha, mkkuu wa mkoa wa Singida, Dk. Parseko Kone aliagiza wakuu wa wilaya na sekretarieti ya mkoa kumaliza tatizo hilo haraka, pia mgogoro wa mpaka kati ya wilaya za Manyoni (Singida) na Sikonge (Tabora). MWISHO.

Sunday, 11 May 2014

ELIMU INAWEZA KUMKOMBOA BINADAMU, HASA KAMA ATAZINGATIA IPASAVYO MASOMO YAKE. JULIUS CHARLES NI MWANAFUNZI WA DARASA LA SITA ANAYETUMIA MGUU WAKE WA KULIA KUANDIKA DARASANI KUTOKANA NA ULEMAVU ALIONAO WA MIKONO.

WANAFUNZI wa Shule ya Msingi Ikungi Mchanganyiko, kitengo cha walemavu (wasioona) wakiwa darasani kuendelea na masomo chini ya walimu wao.
MWANAFUNZI Julius Charles mlemavu wa mikono, akiwa darasani huku akiandika kwenye daftari lake kwa kutumia vidole vya mguu wake wa kulia.
Julius akitandika kitanda chake kwa kutumia mguu wake wa kulia.
Akiwa kwenye darasa la kawaida (mbele aliyeweka daftari chini huku akiandika),pamoja na wanafunzi wenzake wasiokuwa na ulemavu.
Julius akitoka darasanibaada ya kumaliza kipindi na wanafunzi wenzake wasiokuwa na ulemavu.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Olvary Kamilly akiwa ofisini kwake, akizungumza na mwandishi wa habari hizi (hayupo pichani), alisema jamii ya walemavu inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo wazazi kuwaficha majumbani, pia kuwahudumia watu wa aina hii ni gharama kubwa na akaiomba jamii kuisaidia shule hiyo kwa hali na mali.
Singida. Mei 12, 2014. KUNA methali isemayo ‘Shida huleta maarifa’ na ‘Kama hujafa hujaumbika.Julius Charles (12) ni mlemavu wa viungo, anayesoma shule ya msingi Ikungi mchanganyiko, iliyopo Wilaya Ikungi, Mkoani Singida. Ni mlemavu wa mikono, lakini kutokana na bidii darasani ameweza kumudu vyema kusoma na kuandika, hali inayomwezesha awazidi hata wenzake wazima anaosoma nao darasa la sita. Alianza elimu ya msingi mwaka 2006 kwa msaada wa mama yake aliyepata taarifa juu ya shule hiyo yenye kuchukua wanafunzi Mchanganyiko (yaani wenye afya njema) na walemavu ambao wanaishi bweni. Julius alizaliwa kijiji cha Mgungari Wilaya Bunda mkoani Mara mwaka 2002, ni mtoto wa kwanza wa bwana na bibi Charle Namwanga, lakini baba yake aliugua ugonjwa wa akili, hivyo kumtegemea zaidi mama yake, serikali na wahisani kupata mahitaji muhimu. Anamudu vyema masomo yake kutokana na ushirikiano wa walimu tangu akiwa darasa la kwanza, na sasa wenzake na walimu humsaidia kwa kukamatisha kalamu kwenye mguu wa kulia, naye huandika vyema hata kuwazidi wengine wenye mikono kamili. Licha ya kufanya vyema darasani na kushika nafasi ya tatu kati ya wanafunzi 62, Julius pia humudu kuoga na kufanya kazi nyinginezo ndogondogo, ikiwemo kutandika kitanda, lakini anatoa somo kwa walemavu kujiendeleza kimasomo ili baadaye wajikomboe kiuchumi. Kama walivyo watu wengine wenye malengo ya baadaye, ndoto ya Julius ni kuwa mwanasiasa aliyebobea, ili aweze kuwasemea walemavu wenzake akiwa bungeni. Olivary Kamilly ni mwalimu mkuu wa shule hiyo, anasema Julius ni mwanafunzi anayezingatia masomo na hushiriki madarasa yote mawili, akianza na la kawaida, kisha baadaye darasa la walemavu, ingawa pia changamoto zipo nyingi zinazoikabili shule hiyo. Mwalimu Kamilly anaiomba jamii kuacha kuwatenga watoto wenye ulemavu, badala yake wawathamini na wajitahidi kuwasomesha katika shule maalumu, ili baadaye waweze kukidhi matarajio yao. Pia ameiomba jamii kuisaidia shule hiyo ili iweze kumudu vyema kuwahudumia wanafunzi wenye matatizo ya ulemavu. Adamu Bilali ni mwalimu mlemavu wa macho na Anna Mjema ni mwalimu wa wanafunzi wenye ulemavu katika shule hiyo, wanasema kuwa jamii hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo ugumu wa kufundisha mlemavu kama huyu. MWISHO.

MBUNGE WA SINGIDA MASHARIKI TUNDU LISSU AKIWA AMEFUATANA NA MBUNGE WA ARUSHA MJINI GODBLESS LEMA AFANYA MKUTANO IKUNGI NA KUVALISHWA MGOLOLE NA KUPEWA MKUKI IKIWA NI ISHARA YA MTU SHUJAA.

WANANCHI wa Ikungi, Jimbo la Singida Mashariki wakimsikiliza Mbunge wa Jimbo hilo Tundu Lissu alipozungumza na Wananchi hao kwenye mkutano wa hadhara kuzungumzia mambo mbalimbali ikiwemo kuwashaishi vijana na wanawake kujiandika kwenye daftari la kudumu la kupigia kura.
TUNDU Lissu akiwa juu nya jukwaa kuwahutubia wananchi waliojitokeza kusikiliza hotuba yake aliyoitoa makao makuu ya wilaya Ikungi.
. AKILAKIWA na wananchi baada ya kuvikwa vazi la mgolole na kupewa ngao na mkuki ikiwa ni ishara ya mtu shujaa.
Singida Mei 12, 2014. MBUNGE wa Singida Mashariki Tundu Lissu amehimiza vijana, wanawake na walemavu kuzikabili changamoto zilizopo jimboni mwake kwa kujiandikisha kwa wingi kwenye daftari la kudumu la kupigia kura na kuwania nafasi balimbali za uongozi, ili watatue kero hizo wakiwa madarakani. Akizungumza na wananchi wa Ikungi Mjini, Mbunge huyo aliyeingia madarakani kupitia uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 kwa tiketi ya CHADEMA, Lissu alisema kuwa sasa umefika wakati kwa makundi hayo kuwania uongozi, badala ya kuwaachia watu wachache kujirudia kila chaguzi. “Ndugu zangu, hasa vijana na wanawake muda ukifika wa kujiandikisha hakikisheni mnatumia vizuri nafasi hii…tusione aibu kugombea nafasi hizi, tukishinda vizuri nafasi ya vitongoji, vijiji na mitaa itaturahisishia pia kushinda uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na Rais hapo mwakani,”alisema Lissu. Aidha Lissu aliyechaguliwa mwishoni mwa wiki iliyopita na kiongozi wa kambi ya upinzani Freeman Mbowe kuwa waziri kivuli, wizara ya katiba na sheria (muungano), alisema wajumbe wa bunge la katiba kutoka upinzani hawatarudi kujadili muswada wa katiba, hadi hapo lugha chafu za matusi zitakapokoma bungeni. Mapema kwenye mkutano huo mbunge wa Arusha mjini Godbless Lema aliyefuatana na Lissu, aliwaeleza wananchi waliokusanyika makao makuu ya Wilaya ya Ikungi kuendelea kumpa ushirikiano mbunge wa jimbo hilo, ili aendelee kuwapigania. “Mbunge wenu ni mbunge wa taifa, mpeni nafasi afanye kazi ya kuwakomboa watanzania…akienda sehemu mbalimbali za nchi akasimama na kuzungumza, wananchi watamsikiliza na kumuelewa kwa sababu ni mtu wa watu, mpeni nafasi afanye kazi ya kuwatetea wananchi,”alisema. Katika ziara hiyo, Lissu alipokewa na wananchi wa jimbo lake katika kijiji cha Ulyampiti wilaya Ikungi akitokea bungeni Dodoma, na kuvishwa mgolole na akina mama kisha wazee wanaume wakamkabidhi ngao na mkuki, ikiwa ni ishara ya mtu shujaa. MWISHO.

Wednesday, 7 May 2014

HALMASHAURI YA WILAYA MKALAMA YAPITISHA TASIMU YA SHERIA NDOGO KWA AJILI YA ADA NA USHURU KUONGEZA UFANISI WA UTEKELEZAJI WA KAZI ZAKE.

MWENYEKITI wa halmashauri Wilaya Mkalama Mkoani Singida James Mkwega akisisitiza jambo wakati wa maamuzi juu ya kupitisha rasimu ya sheria ndogo mbalimbali,ikiwemo ushuru wa kuku, samaki na mazao, wakati wa baraza la madiwani lililokutana makao makuu ya Wilaya hiyo, Nduguti.
Mwanasheria wa halmashauri ya Wilaya Mkalama Neto Mwambalasu akiwasilisha rasimu ya sheria ndogo ya ada na ushuru mbalimbali mbele ya baraza la madiwani kwenye kikao cha baraza hilo lililokutana makao makuu ya wilaya hiyo, Nduguti.
Baadhi ya madiwani wa halmashauri ya Wilaya Mkalama wakipitia makablasha yenye taarifa mbalimbali ikiwemo rasimu ya sheria ndogo kwa ajili ya ada na ushuru wa kuku, mazao na samaki ili kuiongezea halmashauri hiyo uwezo wa kutekeleza majukumu yake.
Singida Mei 07, 2014. ILI kuiongezea uwezo halmashauri ya wilaya Mkalama Mkoani Singida itaanza kutoza ushuru wa kuku,samaki na mazao mbalimbali. Mwanasheria wa halmashauri hiyo Neto Mwambalasu aliwaeleza wajumbe wa mkutano wa baraza la madiwani lililokutana Nduguti kuwa, utekelezaji wa ushuru huo utaanza kutozwa baada ya kusainiwa na waziri mwenye dhamana, waziri mkuu Mizengo Pinda. Hata hivyo baadhi ya madiwani walionyesha wasiwasi kuhusiana na ushuru wa kuku, lakini mwansheria huyo aliwatoa mashaka kwa maelezo kuwa, sana sheria hiyo itawahusu wafanyabiashara wanaonunua na kusafirisha au kuvusha nje ya Wilaya hiyo. “Nawaomba sana waheshimiwa msipate wasiwasi kuhusiana na rasimu hii…mfano!, ushuru wa kuku wa Sh.500 kwa kuku, hautamhusu moja kwa moja mwananchi wa kawaida, badala yake utahusisha zaidi wafanyabishara wanaonunua na kusafirisha kuku wengi, kwa ajili ya biashara,”alifafanua. Mazao mengine yanayoingia kwenye rasimu na kiwango kikiwa katika mabano ni, samaki aina ya perege (Sh. 300), kambale (Sh. 50), kamongo (Sh.50), ng’ombe, nguruwe na punda (Sh. 2,000), wakati mbuzi na kondooo watalazimika kulipiwa ushuru wa Sh.1,000, kwa mmoja. Kwa mujibu wa Mwansheria huyo, baadhi ya ada na ushuru huo mwingine utakaohusisha maeneo 18, ni mazao ya chakula na biashara, vizimba sokoni, machinjio, ushuru wa madini, ada ya idhini ya ujenzi, mazao ya nyuki na ushuru wa kupaki/kuegesha magari. Katika hatua nyingine, baraza hilo lilipitisha mapendekezo ya kuyagawanya baadhi ya maeneo kwa kuyapandisha hadhi, ikiwemo vitongoji, vijiji, kata na tarafa, ili kutoa fursa kwa wananchi kunufaika na huduma bora baada ya kusogezwa karibu zaidi. Baadhi ya maeneo yaliyopendekezwa kuwa kata ni Mkalama, Nkalakala, Kidarafa, Tatazi, Lukomo, Tumuli, Lyelembo, Ikungu, Kinampundu, Nkungi, Dominiki na Endasiku, wakati tarafa zitakazoongezeka ni Mwanga, Gumanga na Mkalama (iliyobadilishwa kutoka Ibaga kuwa Mkalama). MWISHO.